
Baada ya taarifa ya Jeshi la Polisi na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo juu ya uharibifu uliofanywa kwenye mechi iliyopita ya Kombe la Shirikisho Afrika, kati ya Simba na CS Sfaxien.
Simba imesema ‘Tarehe 15 Desemba 2024, katika mchezo wake wa hatua ya makundi ya kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Cs Sfaxien ya Tunisia katika uwanja wa Benjamin Mkapa, zilizuka ghasia zilizoanzishwa na timu pinzani licha ya kupokelewa na kupewa ushirikiano mkubwa wa maandalizi na wao kusifia mapokezi na ukarimu wetu.
Mara baada mchezo kumalizika Wachezaji, Benchi la ufundi la CS Sfaxien pamoja na Viongozi wake walivamia uwanja na kuanza kuwashambulia waamuzi kitendo ambacho kilifanya wahudumu wa mechi (Stewards) pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama (Polisi) kusaidia kuwaokoa waamuzi hao na kuwatoa uwanjani.

Klabu yetu haikubaliani na vurugu wala uharibifu wa miundombinu katika michezo na hivyo tunaomba na kuwakumbusha mashabiki wetu kuendeleza ukomavu wa kimichezo na kutulia pale ambapo timu pinzani zinapoanzisha fujo dhidi yetu.
Simba itashirikiana na vyombo vya uchunguzi na mamlaka kufanya tathmini ya uharibifu uliotokea katika kadhia hii na tutaendelea kuwa Klabu yenye kusimamia misingi, taratibu na sheria zilizowekwa kwa maslahi ya Taifa letu la Tanzania.
Simba Sports Club imeshiriki mara nyingi katika michezo ya kimataifa na kupelekea kupewa Tuzo ya Mashabiki Bora katika Mashindano ya Ligi ya Afrika, African Football League mwaka 2023.


