Na Daniel Gahu – Katavi.
Katika kuadhimisha siku ya mtoto wa Afrika mkoani Katavi, Mkuu wa wilaya ya Mpanda Jamila Yusuph kwaniaba ya mkuu wa mkoa wa Katavi Mwanamvua Mrindoko amewaelekeza wakuu wa shule, maafisa elimu pamoja na wakuu wa idara za elimu katika mkoa huo kuhakikisha wanaweka sheria za shule ambazo zinatekelezeka ili kulinda usalama wa watoto katika kipindi chote wakiwa shuleni.
Maagizo hayo ameyatoa wakati wa sherehe za maadhimisho ya Mtoto wa Afrika kimkoa yaliyofanyika katika halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika ambapo amesema Serikali inalenga kumlinda mtoto dhidi ya ukatili, ambapo Maadhimisho hayo hufanyika Kila ifikapo tarehe 16 mwezi June Kila mwaka kufuatia tukio la mauaji ya watoto wa shule wapatao elfu mbili katika kitongoji cha Soweto nchini Afrika ya kusini mnamo mwaka 2008.
“Kusimamia maadili na nidhamu itasaidia watoto kuzingatia masomo na kuwaepusha kutumia muda mwingi kufanya matendo ya uovu na pia wazazi endeleeni kuhakikisha ulinzi wa watoto ikiwemo kuwasimamia katika matumizi ya simu, muwaepushe na mitandao ya kijamii, kwani hupelekea ukatili kwa watoto”, Amesema Mhe. Jamila.

Akisoma Risala mbele ya mgeni rasmi Kwa niaba ya wanafunzi wote wa mkoa wa Katavi, Maria Samike amesema zipo changamoto mbalimbali katika jamii ambazo zimefanya watoto washindwe kupata haki za msingi pamoja na kuzifikia ndoto zao.
Miongoni mwa changamoto hizo ameziainisha kuwa ni uelewa mdogo wa jamii juu ya umuhimu wa elimu, umaskini, migogoro ya ndoa inayosababisha wazazi kutengana, mimba za utotoni na ukatili wa kijinsia hasa (vipigo, ubakaji, ulawiti).
“Bado jamii zetu zinaendeleza mila zenye kuleta Madhara, imani za kishirikina na mila potofu ikiwemo chagulaga kwa wasichana ambayo imekuwa ikikatisha ndoto za wasichana wengi,” Amesema Maria.

Kwa upande mkuu wa wilaya ya Tanganyika Onesmo Busweru amesema serikali imewekeza katika kuwajenga walimu na walezi katika kuhakikisha watoto wanakuwa salama. Na amewataka watoto kuitunza na kuitetea serikali na kuwa wazalendo, wasichochewe katika kuleta vurugu watakapokuwa watu wazima na kujitambua.
Katika Maadhimisho hayo, mashirika yakutetea haki za watoto wa mashuleni yakiongozwa na Uwezo Mwakalambo ambaye ni ofisa mwandamizi kutoka VUMA PROJECT amebainisha mradi wao umejikita zaidi katika kutoa elimu ya afya ya uzazi, jinsia pamoja na ujasiliamali kwa watoto waliopo mashuleni.

Pia Nicodemus Luhele, Mkurugenzi mtendaji wa shirika la TOSOVC amebainisha shirika hilo limejikita katika kutoa elimu mbalimbali za makuzi, misaada ya mavazi na vifaa mbalimbali vya shule pamoja na utoaji wa elimu ya afya Kwa watoto.
Maadhimisho siku ya mtoto wa Afrika 2025 yanabebwa na kauli mbiu isemayo Mtoto:Tulipotoka, Tulipo na Tuendako.