Na Saada Almasi – Simiyu.
Wanasiasa nchini wametakiwa kutumia vema majukwaa yao ya siasa kwa kuwa na lugha za staha ili kulinda utu wa kila mtanzania na kuendeleza amani iliyopo nchini
Wito huo umetolewa na Mkuu wa mkoa wa Simiyu, Kenani Kihongosi katika kongamano la kamati za amani za viongozi wa dini kutoka mikoa ya kanda ya ziwa lililofanyika wilayani Bariadi mkoani Simiyu na kuhusisha vyama vya siasa na makundi ya kada mbalimbali na kusema kuwa amani iliyopo nchini inaanzia kwa utu wa mtu.
“angalieni kauli mnazozisema katika majukwaa yenu ya siasa tambua kuwa huyo unayemtamkia maneno mabaya leo ya kuvunja utu wake ana familia anaitwa baba,mama,babu au kaka ,angalia unaweka picha gani kati yako wewe na jamii ambayo inamuheshimu huyo mtu”amesema Kihongosi

Sambamba na hilo Kihongosi amewataka wananchi wa mkoa huo kudumisha amani kwa kuzingatia tunu za taifa hasa katika kuelekea uchaguzi mkuu mnamo Octoba mwaka huu.
“viongozi wetu wa dini wametukumbusha mambo muhimu ya tunu saba za taifa letu niwaombe wananchi wa mkoa huu tuzingatie tunu hizo kwani ndizo muongozo wa amani kuelekea kushiriki uchaguzi mkuu mnamo mwezi Octoba”ameongeza Kihongosi
Naye mwenyekiti wa kamati ya amani mkoa wa Mwanza sheikh Hassan Kabeke amewataka viongozi wa dini kusimama katika nafasi yao na kukemea maovu na kuwakumbusha waamini namna ya kuziishi tunu za taifa kwani uzingatiwaji wake ndiyo unaoleta amani ya nchi.

“viongozi wa dini tunajukumu kubwa la kuwafundisha na kuwakumbusha waamini wa dini zetu kuhusu tunu za taifa ambazo ni utu,uzalendo,uwajibikaji ,umoja ,uwazi na uadilifu kwani ziko ndani ya vitabu vyetu Quran na Biblia na yeyote anayesimama kwa mazingatio haya hakutokuwa na sababu ya kuleta machafuko nchini”sheikh Kabeke
Kwa upande waka sheikh mkuu wa mkoa wa Simiyu sheikh Issa Kwezi amewataka washiriki wa kongamano hilo kuwa mabalozi wazuri kwa wengi ambao hawakupata nafasi ya kukumbushwa juu ya tunu za taifa akisema kuwa kamati hizo zitaendelea kutoa semina kwa makundi mengi zaidi ili wengi wapate kufikiwa

“ushiriki wako hapa ni faida inayokupa sababu ya kudumisha amani ya nchi na ninawaomba mfikishe kwa wengi ambao hawakufika lakini pia huu ni mwanzo mzuri kwa kamati hizi za amani kufika katika maeneo mengi zaidi ili wanufaika waongezeke kuzijua tunu za taifa ili kuendeleza amani tuliyonayo nchini”amesema Kwezi
Kongamano la kamati za amani lilikamilika kwa kuazimia kufikisha ujumbe wa tunu za taifa katika nyumba za ibada sambamba na kuzikfikishia ujumbe taasisi ya TAKUKURU kudhibiti mianya ya rushwa pamoja na TUME ya taifa ya uchaguzi kutenda haki kwa wagombea hasa katika kuelekea uchaguzi mkuu mwezi Octoba mwaka huu