Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Kaster Ngonyani amewaasa wananchi kuwa na ushirikiano na Jeshi la Polisi katika kudhibiti uhalifu na kuwataka watumie Polisi kata waliopo katika maeneo yao katika kutatua changamoto za kihalifu zinazowakabili.
Rai hiyo ameitoa katika mkutano wa hadhara wa Polisi jamii uliofanyika katika kijiji na kata ya Ilunde wilaya ya mlele mkoa wa Katavi ikiwa ni mwendelezo wa utoaji elimu ya usalama kwa wananchi.

“Wananchi ili kudhibiti uhalifu katika maeneo yenu mnapaswa msifumbie macho vitendo hivyo kwa kizingizio cha kusema ulinzi ni jukumu la askari Polisi pekee mnatakiwa kushirikiana na Jeshi la Polisi katika kuwabaini wahalifu kwa kuwatumia Polisi kata waliopo katika maeneo yenu”, alisema SACP Ngonyani.
Kwa upande wake mwenyekiti wa kamati ya usalama na Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mhe. Mwanamvua Mrindoko amewataka wananchi hao kila mmoja katika nafasi yake kutoa taarifa za wahalifu kwa Jeshi la Polisi kwa wakati ili waweze kuendelea kuwa salama.