Viongozi wa sekta ya afya wametakiwa kuwaeleza wananchi mafanikio yanayopatikana katika sekta ya afya ili kufahamu namna serikali ilivyoboresha huduma za afya nchini.
Hayo yamebainishwa Jijini Dodoma na Naibu waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Festo Dugange alipokuwa akifungua kikao kazi cha kujadili utekelezaji wa Mpango wa Afua za Takwimu za Bidhaa za Afya (IMPACT).
Dkt.Dugange amesema kuwa serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Mhe. Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan imefanya uwekezaji mkubwa katika sekta ya afya kwa kujenga vituo vya kutolea huduma za afya,ununuzi wa dawa na vifaa tiba pamoja na kuajiri wahudumu wa afya hivyo ni jukumu la kila kiongozi kuyasemea mafanikio hayo kwa wananchi.
Akizungumzia kuhusu vifaa tiba vilivyonunuliwa na serikali Dkt.Dugange amewaagiza wahudumu wote kuvitunza vifaa hivyo ili viweze kudumu kwa muda mrefu.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu kutoka Ofis ya Rais Tamisemi anayeshughulikia Afya,Ustawi wa Jamii na Lishe Dkt.Charles Mahera amewaagiza waganga wakuu wa mikoa kudhibiti wizi wa vifaa tiba na dawa unaotokea sehemu mbali mbali nchini.