Moja ya changamoto kubwa inayochangia kushuka kwa jitihada Zinazofanywa na Serikali katika Mkoa wa Geita kwenye kupunguza maambukizi ya Virusi vya ukimwi ni imani potofu kwa wazazi na walezi kutokana na watoto wengi kukatiza Matibabu ya dawa za kufubaza virusi hivyo na badala yake kuwapeleka kwa Waganga wa kienyeji ili kupata matibabu ya ugojwa wa ukimwi.
Akizungumza na Jambo FM, kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Geita Dkt. Michael Mashala amesema kutokana na wazazi na Walezi wengi katika Mkoa wa Geita kukabiliwa na changamoto ya kuamini Mtoto akizaliwa na maambukizi ya VVU anakuwa amelogwa hali hiyo imekuwa kikwazo cha kuwakatisha watoto wengi na Matibabu ya dawa za kufubaza VVU na kuwapeleka kwa waganga wa kienyeji kutibiwa.
Katika kukabiliana na changamoto hiyo afisa ustawi wa jamii kutoka Ofisi ya Rais Tamisemi Idara ya Afya Ustawi wa Jamii na Lishe Harun Musa amesema serikali imekuja na mradi wa kizazi hodari unaolenga kutoa elimu, na kuboresha afya kwa watoto wanaoishi na virusi vya ukimwi ili kuhamasisha matumizi ya dawa za kufubaza virusi hivyo.
Kwa upande wake Msimamizi wa Mradi Aminiel Alen amesema Mradi huo unatekelezwa katika Mikoa 9 ya Tanzania bara na unalenga kuwafikia wanufaika zaidi ya elfu 28 katika Mkoa wa Geita kwa lengo la kuimarisha afya na ustawi na ulinzi kwa watoto wanaoishi na maambukizi ya virusi vya ukimwi.