Watu wengi wamekuwa wakiamini kuwa gerezani ni sehemu ya mateso au sehemu ambayo mfungwa hupelekwa ili akatumikie adhabu fulani ila jambo hili kidogo limekuwa tofauti kwa Timoth Kaombwe ambaye kwa sasa ni mkazi wagereza kuu la Butimba Jijini Mwanza.
Timoth ambaye kwa sasa ni raia huru aliwahi kuhukumiwa kifungo cha miaka 30 jela ila baadae akaachiwa huru mwaka 2019, yeye anasema wakati akiwa gerezani alitumia muda wake mwingi kujifunza fani mbalimbali kama vile kilimo na ujenzi shughuli ambazo kwa sasa ndizo zinazomsaidia kuendesha familia yake.
Timoth anasema kupitia fani hizo mpaka sasa ameza kununua kiwanja, kujenga nyumba pamoja na kupata fedha ambazo zimekuwa zikitumika katika kuendesha maisha yake ya kila siku. Aidha pia ametumia fursa hiyo kuwaomba wafungwa wengine hapa nchini kuwa na desturi ya kujifunza fani mbalimbali ili pale wanapotoka gerezani fani hizo ziweze kuwasaidia katika kuendesha maisha ya kila siku.
Kwa upande wake Mkuu wa Gereza la Butimba Jijini Mwanza Justice Kaziulaya amesema gereza la Butimba limekuwa na desturi ya kutoa mafunzo ya fani mbalimbali kwa wafungwa hao lengo kubwa likiwa ni kuwapa ujuzi utakaowasaidia pale wanapomaliza kutumikia adhabu.