Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha ameushauri uongozi wa Chuo cha Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi Shinyanga (VETA) mkoa wa Shinyanga kuanzisha na kusajil iKitengo Maalum cha Kuimarisha Uwezo wa Kujitegemea (Self Reliance Unity) kitakachokuwa na wajibu wa kubuni na kutekeleza kazi mbalimbali kwa kutumia rasilimali walizonazo ikiwemo wanachuo, mitambo na wakufunzi lengo likiwa ni kuzalisha kipato cha chuo huku akisema kuwa Serikali itafanya kazi pamoja nao ikiwa ni pamoja na kuwapatia zabuni za kujenga miradi ya Serikali.
RC Macha ameyasema hayo wakati wa hafla ya Mahafali ya 43 iliyofanyika katika Viwanja vya VETA Shinyanga na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali, Dini, wazazi/walezi, watumishi wa VETA, wananchi na wanachuo wenyewe ambapo pamoja na mambo mengine amewataka wahitimu kwenda kuchangamkia fursa za mikopo ya asilimia kumi anayotolewa na halimashauri isiyokuwa na riba pamoja na kuchapa kazi kwa bidii zaidi.
“Pamoja na pongezi kwako Mkuu wa Chuo na watumishi wote, lakini niwatake sasa kuanzisha Kitengo Maalum cha Kuimarisha Uwezo wa Kujitegemea (Self Reliance Unity) ambacho kitasajiliwa na kutambulika chenye lengo la kuzalisha, kukiwezesha chuo hiki kufanya kazi za nje, kuongeza pato na kukifanya chuo kujitegemea na kuchechemua uchumi wenu kupitia Fani mnazofundisha ikiwemo utengenezaji wa barabara na Serikali itafanya kazi pamoja nanyi na kuwashika mkono kwa kuwa mna kila kitu hapa ikiwemo mitambo mizito ya kutekelezea kandarasi za aina yoyote,” amesema RC Macha.
Awali akitoa taarifa mkuu wa chuo hicho cha elimu ya mafunzo na ufundi stadi katika mkoa wa Shinyanga (VETA) MWALIMU Abraham Mbughuni amesema kuwa VETA Shinyanga ina jumla ya Ekari 19 zenye Hati Miliki, mazingira rafiki, tulivu na yenye kuvutia kwa kufundishia, kujifunzia, kupumzikia, mabweni, vyumba vya madarasa, karakana, maeneo ya kufundishia pamoja na kutoa taaluma kwa fani ya uendeshaji mitambo mizito, magari, uchomeleaji na uunganishaji vyuma huku akiwakaribisha wananchi kuleta kazi zote zinazohusu fani hizo kwani VETA inapokea na kutekeleza kwa ufanisi na weledi mkubwa zaidi.
Chuo cha VETA Shinyanga kilianzishwa rasmi mwaka 1989 kikiwa na fani moja tu ya ujenzi ambapo kwa sasa kina jumla ya wanachuo wa fani za muda mrefu 525 na walimu wamuda mfupi 735 hii ni kwa kipindi cha kuanzia Julai 2024 huku uwezo wa Chuo kuchukua wanachuo unatajwa kuwa 400 wa muda mrefu na 1000 wa muda mfupi.
Uanzishwaji wa Kitengo Maalum VETA Shinyanga unatajwa kuja kuwa mwarobaini na sehemu ya kuongeza ajira kwa wahitimu na wataalam wa fani mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kuchochea uchumi wa Chuo, kuongeza pato la Serikali na kuimarisha taaluma kwa vitendo huku wito ukitolewa na RC Macha kwa wanafunzi hao kutumia muda mwingi kwa vitendo na kupunguza nadharia.
Mwisho RC Macha amependekeza VETA Shinyanga kutumia Kaulimbiu isemayo “VETA SHINYANGA, KAZI MKONONI” badala ya VETA SHINYANGA, DARAJA LA MAFANIKIO”.