Categories

Do you have a Story?

Call us on 0677 644 444 to submit your news story or incident report!

Ushirikishaji wa NGO’s Kusaidia Ripoti za CAG Kufika Vijijini

Imeelezwa kwamba ushirikishwaji wa Asasi za kiraia katika ufikishaji wa elimu kwa jamii za maeneo ya vijijini na jamii kwa ujumla utasaidia kuongeza uelewa na ufuatiliaji wa shughuli zinazofanywa na ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Kaimu Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Nje Mkoa wa Shinyanga Bw. Nahumu Jairo ameeleza hayo kupitia hotuba ya ufunguzi wa warsha ya siku moja iliyofanyika Julai 8,2024 mwaka huu iliyojumuisha asasi 25 za kiraia Mkoani Shinyanga kwa lengo la kuzijengea katika kufautilia na kutumia taarifa za CAG katika utekelezaji wa majukumu yao ambapo pia ametumia nafasi hiyo kuelezea kilichoisukuma ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kushirikisha Asasi hizo.

“Lengo ni kuboresha usambazaji wa ripoti hii ya wananchi na kumfikia kila mwananchi ili aweze kupata taarifa za kiukaguzi,sambamba na usambazaji wa ripoti hii kwa miaka iliyopita,mafanikio tuliyoyapata ni kuweza kufanya kazi pamoja na asasi zisizo za kiraia kwa ukaribu,hii imesaidia kuboresha kazi za ukaguzi ambazo zinasaidia kuleta maendeleo ya nchi kwasababu kila mmoja anajifunza jinsi ya kutumia na kulinda rasilimali ambazo zinatokana na kodi zetu sisi wenyewe” amesema Bw.Nahumu
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini kutoka Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Bw.Focus Mauki anaeleza kuhusiana na toleo maalum la Mwananchi kutoka katika ofisi hiyo.

“Toleo Maalum la Mwananchi ni kitabu ambacho kina mkusanyiko wa taarifa kuu za Mdhibiti na Mkaguzi mkuu wa Serikali,sasa kitabu hicho huwa tunakiandaa katika lugha ambayo tunasema ni nyepesi ili mwananchi apate kufahamu”ameeleza Bwana Mauki

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali Mkoa wa Shinyanga Bw.Mussa Jonas Ngangala amesema kwamba warsha hiyo imetoa funzo kubwa kwa wadau wa mashirika yasiyo ya kiraia na kueleza kwamba yamewezesha kujua namna bora ya kufanya maandiko mazuri kwa kuzingatia kilichoibuliwa na kuandikwa katika ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali(CAG).

“Tunashukuru sana Ofisi ya CAG kutufikia katika Mkoa wa Shinyanga na kuwalenga wadau wanaotoka katika Sekta ya NGO’s,sekta ya NGO’s ni sekta pana inayokuwa karibu na Wanajamii na wananchi kwa ujumla na ni sekta inayotoa elimu mbalimbali kwenye makundi mbalimbali huko kwenye jamii na ndiko ilikojikita katika kufanya kazi kwahiyo mafunzo haya yametoa funzo kubwa sana na imetupa urahisi sisi sasa kwenda kutoa elimu huko kwenye Jamii kuhusiana na ofisi ya CAG na Majukumu yake na namna inavyofanya kazi na namna inavyofanya ukaguzi katika taasisi hizi za umma”. Amesema Bw.Ngangala

Baada ya Warsha hiyo kukamilika,John Myola,Cecilia Msangwa na Eliasenya Nnko ambaoni baadhi ya washiriki kutoka katika Asasi hizo 25 wamekuwa na maoni mbalimbali ikiwa ni pamoja na kupongeza kazi zinazofanywa na Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali(CAG),kuoimba serikali na mamlaka husika kuchukua hatua kwa wale waote wanaomulikwa na kubainika kuhusika na ubadhirifu wa mali na fedha za umma pamoja na kueleza kwamba mafunzo waliyoyapata kupitia warsha hiyo yatakuwa na matokeo chanya ya kwa kuwezesha lengo la kufikisha yaliyomo katika toleo Maalum la Mwananchi la Ripoti za Ukaguzi kwa mwaka wa fedha 2022|2023 ndani ya jamii.

Miongoni mwa mada zilizowasilishwa na kujadiliwa kupitia warsha hiyo ni pamoja na mpango Mkakati wa Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi,Ripoti ya Ukaguzi wa Serikali Kuu,Ripoti ya Ukaguzi wa Serikali za Mitaa, hati za Ukaguzi ,Ripoti ya Mifumo,Ripoti ya Ukaguzi wa Miradi na Ukaguzi wa Ukaguzi wa Mashirika ya Umma pamoja na Ripoti ya Ufanisi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *