UFUGAJI WA SAMAKI KWA NJIA YA VIZIMBA WACHAGIZA UCHUMI WA WANANCHI KAGERA

Na Clavery Christian – Kagera.

Mkoa wa Kagera, umeendelea kung’ara katika sekta ya uvuvi na ufugaji wa Samaki kupitia mbinu ya kisasa ya vizimba kwenye Ziwa Victoria.

Ufugaji huo, huwezesha uzalishaji mkubwa wa samaki kwa muda mfupi, pia unarahisisha usimamizi wa afya ya samaki, usafi wa mazingira, na utoaji wa lishe bora kwa samaki, jambo linaloongeza uzalishaji na ubora wa samaki wanaovunwa.

Afisa Uvuvi Mkoa wa Kagera, Efrazia Mukama amesema teknolojia hiyo inawezesha ukuaji Samaki ndani ya vizimba vinavyoelea juu ya maji ya ziwa, badala ya kutumia mabwawa au mito ya asili.

Amesema, Mradi huo unatekelezwa katika maeneo ya Rubafu na Kyamalange, ndani ya Wilaya ya Bukoba Vijijini, ambapo vikundi vya vijana na wanawake kama (17) vimepokea mafunzo, vifaa, na vifaranga kwa ajili ya kuanzisha vizimba vya ufugaji.

Mukama amesema vikundi hivyo 17 na watu binafsi watano, tayari wamenufaika na mikopo ya Serikali isiyokuwa na riba kwa ajili ya ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba.

Mradi huo, unasimamiwa kwa karibu na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na TAFIRI, pamoja na mashirika ya kimataifa kama FSD Africa na TACT.

Serikali ya Mkoa wa Kagera kupitia ofisi za Halmashauri imekuwa ikihamasisha wananchi kujitokeza kuchangamkia fursa hii mpya.

Aidha, Mukama amesema mradi unakabiliwa na changamoto kama gharama kubwa za kuanzisha vizimba, upatikanaji wa chakula cha samaki, pamoja na uvuvi haramu unaoathiri maendeleo ya shughuli za ufugaji.

Ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba umejionesha kuwa suluhisho la kuongeza kipato cha wananchi wa mkoa wa Kagera, kupambana na umaskini, na kukuza ajira hasa kwa vijana.

Kwa usimamizi madhubuti, fursa hii inaweza kuwa chachu ya maendeleo endelevu katika ukanda wa Ziwa Victoria na Tanzania kwa ujumla.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *