SIDO YAENDELEZA USAIDIZI KWA WAJASIRIAMALI WABUNIFU

Wizara ya viwanda na biashara kupitia SIDO imeendelea kuwasaidia wajasiriamali wenye ubunifu wa teknolojia na mawazo ya bidhaa mpya kwa kuwapa huduma wezeshi ikiwa ni pamoja na maeneo ya kufanyia kazi, ushauri wa kiufundi na mitaji ili wakue na kufikia viwango vya kujitegemea.

Hayo yamebainishwa Jijini Dodoma na Waziri wa Viwanda na Biashara, Seleman Jafo wakati akielezea mafanikio ya Wizara hiyo katika kipindi cha miaka sita ya Uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambapo amesema hadi kufikia Machi, 2025 mawazo bunifu matatu yamehitimu katika Mkoa wa Arusha, Dar es salaam na Kilimanjaro.

“ Mawazo hayo bunifu ni utengenezaji wa mbolea kutokana na nywele za binadamu, mashine ya kukatakata mchaichai kwa ajili ya kusindika, na mashine ya kurutubisha unga”, amesema

“Aidha, mawazo bunifu 22 kutoka kwa wabunifu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mbeya, Arusha, Mwanza, Singida na Morogoro yanaendelea kuatamiwa.” Amesema Jafo.

Vilevile amesema katika kuwaendeleza na kuwawekea mazingira rafiki wabunifu, Wizara kupitia SIDO imeingia makubaliano na Tume ya TEHAMA kwa ajili ya kuboresha Kituo cha Uatamizi Jijini Dar es Salaam.

Hali kadhalika amesena moja ya makubaliano hayo ni kukarabati vituo vya uatamizi katika Mikoa ya Dar es Salaam, Mbeya, Arusha, Mwanza, Lindi na Tanga.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *