Baada ya kusambaa kwa video ya Mwindaji wa Marekani, Josh Bowmer akifurahia kuwinda mamba mkubwa nchini Tanzania mwenye rekodi ya dunia na kuleta taharuki, Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori (@tawa_tanzania ) imesema inaendelea na uchunguzi kuona kama kuna ukiukwaji wa Sheria za uwindaji.
Taarifa ya TAWA imesema mara baada ya uchunguzi kukamilika taarifa kamili itatolewa na hatua za kisheria zitachukuliwa iwapo ukiukwaji utabainika.
“TAWA inapenda kufahamisha Umma kuwa uwindaji wa kitali hufanyika kwa kuzingatia sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori sura ya 283 pamoja na kanuni za uwindaji wa kitalii za mwaka 2015 na marekebisho yake ya mwaka 2017, 2019 na 2020, uwindaji wa kitalii pia husimamiwa na Mkataba wa Kimataifa wa Biashara ya Wanyamapori na Mimea iliyohatarini kutoweka (Convention on International Trade In Endangered Species of Wild Fauna and Flora – CITES) ambao Nchi yetu imeridhia.
“Mamba ni miongoni mwa wanyamapori wanaolindwa na mkataba huu na wamewekwa katika kundi la pili (Appendix II) ambalo linaruhusu matumizi ya uvunaji ikiwemo windaji wa kitalii, masharti ya uwindaji wa mamba kwa muibu wa Kanuni na Mkataba wa CITES ni kuhakikisha mamba wote wanaowindwa chini hawazidi 1,600 kwa mwaka, mamba anavewindwa ana urefu usiopungua sentimita 300, vibandiko maalum (Skin tags) vinafungwa katika ngozi za mamba wanaowindwana (iv) Vibali vya CITES (CITES export permit) vinatumika kusafirisha nyara zitokanazo na mamba waliowindwa” imeeleza taarifa ya TAWA.
“Chini ya Sheria na Mkataba huo, Mtu yeyote anaruhusiwa kufanya uwindaji wa kitalii baada ya kupata kibali kutoka TAWA na kutimiza masharti kama ilivyobainishwa hapo juu, TAWA inawajibu wa kusimamia uwindaji huo katika hatua zake zote, kumbukumbu tulizonazo zinaonyesha kuwepo kwa vibali vya uwindaji wa wanyamapori ikiwemo mamba katika maeneo mbalimbali nchini” — TAWA