Categories

Do you have a Story?

Call us on 0677 644 444 to submit your news story or incident report!

Serikali yatenga Trioni Moja kununua dhahabu nchini.

Na Costantine James

Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BOT) imetenga fedha kiasi cha shilingi trioni 1 kwa ajili ya ununuzi wa dhahabu hapa nchini hali itakayowawezesha wachibaji wa dhahabu, wachenjuaji pamoja na wafanyabishara kunufaika zaidi na sekta ya madini.

Hayo yamebainishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati akifunga maonesho ya Saba ya kitaifa ya teknolojia ya Madini 2024 Mkoani Geita ambapo amesema serikali imeamua kununua dhahabu hizo na itanunua kwa bei kubwa kulinganisha na bei ya soko ili kuwafanya wachimbaji pamoja na wafanyabiashara kunufaika zaidi na sekta ya madini.

Rais Samia amesema ununuzi wa dhahabu hizo unaofanywa na Benki Kuu ya Tanzania (BOT) utakuwa na manufaa makubwa zaidi kwa wachimbaji pamoja na wafanyabiashara mbalimbali wa madini kwani katika ununuzi huo serikali imetoa msamaha wa kodi kwa wachimbaji na wafanyabiashara wa madini wakati wa uuzaji wa dhahabu kwa BOT.

Rais Samia ameongeza kuwa sekta ya madini imekuwa ni sekta muhimu katika kuchangia pato la taifa kwani kwa sasa sekta hiyo inachangia asilimia 9 ya pato la taifa na ikifikapo 2025 sekta ya madini itachangia asilimia 10 ya pato la taifa kutokana na mikakati mbalimbali inayofanywa na serikali katika kuimarisha sekta ya madini hapa nchini.

Akizungumza katika hafla ya ufungaji wa maonesho hayo Waziri Madini Antony Mavunde amesema serikali imefuta zaidi ya leseni 2000 ambazo zilikuwa zimehodhiwa na watu wachache na sasa serikali inakwenda kuzigawa leseni hizo kwa wachimbaji wa wadogo kwa kufata utaratibu huku akisema serikali haitasita kufuta leseni ambazo wamiliki wake hawaziendelezi.

Akitoa taarifa ya maonesho hayo mbele ya Rais Samia Mkuu wa Mkoa wa Geita Martine Shigela amesema maonesho hayo yalianza October 2, 2024 ambapo yametamatika October 13, 2024 na washiriki zaidi ya 600 wameshiriki na kuwafanya wachimbaji wa madini kunufaika zaidi kwa kujifunza teknolojia mpya za uchimbaji huku akisema Mkoa wa Geita umetenga zaidi Milioni 100 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa mabanda ya kudumu katika uwanja huo ili kuyafaya maonesho hayo kuwa ya kimatifa.

Kwa upande wake Rais wa shirikisho la wachimbaji Tanzania (FEMATA) Johna Bina ameipongeza serikali kwa namna ambayo inafanya jitihaa za kuiimarisha sekta ya madini ambapo mabadiliko makubwa yanaonekana kila kukicha huku akiiomba serikali kuondoa kodi kwenye vifaa vya uchimbaji vinavyoingizwa na wachimbaji wadogo hapa nchini kwa ajili ya uchimbaji hali itakayosaidia kuchochea matumizi ya teknolojia katika uchimbaji wa madini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *