Dkt. Biteko aongoza wananchi wa Bukombe Kujiandikisha Katika Daftari la Wapiga Kura

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Bukombe Mkoani Geita, ametoa wito kwa wananchi wa Bukombe na Tanzanaia kwa ujumla kujitokeza kwa wingi kujiandikisha kwenye Daftari la Wapiga Kura ili waweze kushiriki kikamilifu katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27, 2024.

Akizungumza leo, Oktoba 11, 2024, baada ya kujiandikisha katika Kituo cha Shule ya Msingi Bulangwa, Wilaya ya Bukombe, Dkt. Biteko amewataka wananchi kutumia muda huu fupi wa kujiandikisha kwa manufaa ya ushiriki wao katika uchaguzi.
“Nawashukuru sana kwa kujitokeza kwa wingi. Zoezi la kujiandikisha ni la haraka, hivyo nina imani kuwa mtamaliza kwa wakati na kurejea kwenye shughuli zenu za kila siku,” Dkt. Biteko.

Amesisitiza kuwa: “Zoezi hili litaendelea hadi Oktoba 20, 2024, hivyo ni muhimu wananchi wa Bulangwa mjitokeze kwa wingi. Waandikishaji wapo tayari, na tunataka kuhakikisha kila mwenye sifa ameandikishwa, ili siku ya uchaguzi ifike, kila mmoja aweze kupiga kura kwa haki.”

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigella, amempongeza Dkt. Biteko kwa kuwa mfano wa kuigwa kwa wananchi wa Bukombe nakueleza umuhimu wa kila mmoja kutumia haki yake ya kikatiba kwa kujiandikisha na kushiriki uchaguzi wa serikali za Mitaa.

“Tuendelee kuhamasisha wananchi kutoka kila kona ya jimbo kujiandikisha. Tumetenga maeneo ya kutosha ili kila mmoja mwenye sifa apate fursa ya kuandikishwa kwa urahisi,” amesema Shigella.

Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe, Bw. Lutengano Mwalyibwa amesema kuwa maandalizi ya zoezi hili yamekamilika, huku akisema Wilaya ya Bukombe ina vituo 348 vya kujiandikisha, na wanatarajia kuandikisha wapiga kura 109,124.

✍ Costantine James

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *