Rais Samia Suluhu Hassan amemuelekeza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuwa serikali igharamie mazishi ya watu wote waliopoteza maisha kutokana na mafuriko katika Wilaya ya Hanang.
Taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu iliyotolewa leo Disemba 4, 2023 imesema Rais Samia pia ametaka majeruhi wote waliopo kwenye hospitali mbalimbali wapate matibabu yote yanayostahili kwa gharama za serikali.
Aidha, Rais Samia ameelekeza serikali ya Mkoa wa Manyara na Kitengo cha Maafa cha Ofisi ya Waziri Mkuu, kuhakikisha wananchi wote ambao makazi yao yamesombwa na maji, wapate makazi ya muda.
Hadi sasa, idadi ya waliofariki kutokana na janga hilo la mafuriko imefikia watu 50 huku kaya zilizoathirika zikiwa ni zaidi ya 1,100 na kuathiri watu zaidi ya 5,000 huku ekari 750 za mashamba zikiwa zimeharibika.