Paul Pogba amefungiwa kucheza soka miaka minne

Kiungo wa Juventus na timu ya taifa ya Ufaransa, Paul Pogba amefungiwa kucheza soka miaka minne baada ya kugundulika kuwa anatumia dawa za kusisimua misuli.

Pogba alipimwa na kukutwa na kiwango cha juu cha homoni ya Dehydroepiandrosterone (DHEA) homoni ambayo huchochea uzalishaji wa testesterone mwezi Agosti mwaka jana.

Mahakama ya Kitaifa ya Kupambana na Matumizi ya Madawa ya Kulevya nchini Italia (TNA) ilikubali ombi la ofisi ya mwendesha mashtaka wa kupambana na dawa za kulevya la kutoa kifungo cha miaka minne ambacho ni cha kawaida kwa mujibu wa kanuni ya dunia ya kupambana na dawa hizo.

Pogba alianza kutumikia adhabu hiyo tangu alipopimwa kwa mara ya Kwanza Agosti 2023, hivyo atakuwa nje ya uwanja hadi Agosti 2027. Mwaka ambao atakuwa na umri wa miaka 35 suala ambalo limewaumiza kichwa mashabiki wake ikiwa bado ataendelea kusakata kabumbu baada ya kifungo hicho.

Kwa mujibu wa taarifa zilizopo, kiungo huyo atakata rufaa dhidi ya uamuzi huu kwenye Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (CAS).

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *