Jopo la madaktari limetumia jumla ya saa mbili kuwafanyia upasuaji wa kurekebisha maumbo wa wanawake wanne kwa lengo la kupunguza uzito katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili-Mloganzila, jijini Dar es Salaam.
Hata hivyo, mwanaume mmoja aliyekuwa kwenye orodha hiyo hakuonekana leo, Oktoba 28, 2023, ikiwa ndiyo siku ambayo hospitali hiyo imeanza kutoa huduma hiyo kwa mara ya kwanza nchini.
Akizungumza baada ya zoezi hilo kufanyika, Mkuu wa Idara ya Upasuaji katika Hospitali hiyo, Dk Erick Muhumba amesema kutokana na hali zao kuendelea vizuri, wanawake hao wanatarajiwa kuruhusiwa kutoka wodini kesho, Jumapili.
