Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga imepanda miti zaidi ya milioni 1.2 katika kipindi cha mwaka 2023 kati ya miti milioni 1.5 iliyopaswa kupandwa katika kila halmashauri nchini ili kutekeleza agizo lililotolewa na serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira.
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Shinyanga, Elias Ramadhani Masumbuko ametoa takwimu hizo aliposhiriki zoezi la upandaji wa miti pembezoni mwa mto Kidalu kata ya Ibinzamata lililoratibiwa na shirika la utangazaji Tanzania na kutumia fursa hiyo kueleza juu ya malengo waliyojiwekea katika upandaji wa miti.
Mwakilishi wa Shirika la Habari Tanzania mkoa wa Shinyanga Bw.Greyson Kakuru ameeleza kuhussiana na kilicholisukuma shirika hilo kwa kushirikiana na waandishi wa habari,wananchi na viongozi kupanda miti katika Manispaa ya Shinyanga.
Kwa upande wake Msimamizi wa Idara ya maliasili na Mazingingira Manispaa ya Shinyanga Bw.Ezra Manjelenga ameeleza kuhusiana na hatua zinazochukuliwa katika utekelezaji wa agizo la serikali kuu katika kuhakikisha miti milioni 1.5 inapandwa katika Manispaa ya Shinyanga.
Hadi kukamilika kwa mwaka wa fedha 2022|2023, ni halmashauri 23 tu kati ya 184 ambazo ni sawa na asilimia 12.5 zilifanikiwa kutekeleza kikamilifu lengo la kupanda miti milioni 1.5 kwa kila halmashauri ambapo kwa mkoa wa Shinyanga ni halmashauri ya Ushetu pekee iliyokuwa imefikia lengo hilo.