Magari 127 Hayajatengenezwa Wala Kuuzwa Katika Halmashauri 13

Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere(Ripoti kuu ya Ukaguzi wa Serikali za Mitaa ),kwa mwaka wa fedha wa 2022/23, inaeleza kwamba baada ya CAG kufanya tathmini ya udhibiti wa mifumo ya ndani, hasa kuhusiana na magari kwa kupitia rejista ya utunzaji, matengenezo pamoja na rejista ya mauzo ya magari,alibaini kuwa mamlaka 13 za serikali za mitaa zilikuwa na jumla ya magari mabovu 127 ambayo yameachwa bila kufanyiwa huduma za matengezo au kuuzwa kulingana na taratibu za uuzaji wa mali za umma.

Hali hiyo ni kinyume na agizo la 45(1) la Memoranda ya fedha za serikali ya mwaka 2009. Kutotengeneza magari kunaweza kuongeza uchakavu na kufupisha muda wa matumizi ya magari husika, hivyo manufaa yaliyotarajiwa kutopatikana.

CAG ameeleza hali hiyo kuwa pia inaweza kupunguza utekelezaji wa shughuli ambazo zilipaswa kuwezeshwa na magari hayo na matokeo yake ni kuzorotesha utendaji wa uendeshaji wa halmashauri husika.

Halmashauri zilizokutwa na dosari hii ni pamoja na halmashauri ya wilaya ya Mpimbwe yenye magari matano, wilaya ya Mtama magari na pikipiki 34, halmshauri ya wilaya ya Mvomero Magari 9, wilaya ya Rufiji magari 8, Ulanga magari 19, halmashauri ya wilaya ya Itilima magari manne na halmashauri ya wilaya ya Ludewa magari 12 ambayo hayakutengenezwa wala kuuzwa.

Halmashauri nyingine ni wilaya ya Kibiti yenye magari mawili,halmashauri ya wilaya ya Geita magari matatu,Wilaya ya Wanging’ombe magari matatu,Busokelo magari matano(05),halmashauri ya wilaya ya Mbeya magari 16 na halmashauri ya wilaya ya Rungwe Magari 7.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *