Wazazi wameaswa kufuatilia michezo ya watoto kwa karibu zaidi na kuwazuia kuweka vitu mdomoni, puani pamoja na masikioni ili kuwaepusha na madhara mbalimbali ikiwemo madhara ya kudumu na kifo, kauli hiyo imetolewa na jopo la madaktari bingwa wa upasuaji wa kifua na moyo, mapafu na mfumo wa upumuaji wa hospitali ya taifa muhimbili ambao wameshiriki kuondoa shanga ya plastiki iliyokuwa imekwama katika pafu la kulia la mtoto mwenye umri wa miaka mitano.
Daktari bingwa wa mapafu na mfumo wa upumuaji, Dkt. Mwanaada Kilima amesema, shanga hiyo iliingia kwenye pafu baada ya kumpalia mtoto alipokuwa akiichezea mdomoni takribani mwezi mmoja uliopita.
Dkt. Kilima amesema mtoto huyo alitaabika tangu wakati huo kwa kikohozi na kupumua kwa shida huku njia mbalimbali zikitumika kujaribu kuitoa na kugonga mwamba, ndipo wataalamu wa mapafu walipofanikiwa kuitoa bila madhara yoyote.