Frank Aman – Geita.
Wakala wa Majisafi na Usafi wa Mazingira Vijijni (RUWASA) Wilaya ya Geita, imeweka wazi kuwa imefikia asilimia 60 ya utekelezaji wa mradi maalum wa visima vitano vya maji wemajimboni.
RUWASA inatekeleza mradi wa visima 10 vya maji kwenye majimbo mawili ya halmashauri ya wilaya ya Geita, kwa mgawanyo wa visima vitano kwa jimbo la Busanda na visima vitano Geita vijijini.
Meneja wa Ruwasa Wilaya ya Geita, Mhandisi Sande Batakanwa ametoa taarifa hiyo Juni 10, 2025 alipotembelea na kukagua maendeleo ya mradi katika kijiji cha Buyagu jimbo la Busanda.

Amesema mradi huo ni sehemu ya programu ya visima 900 Tanzania bara chini ya serikali ya Rais Dk Samia Suluhu Hassan ambaye amelenga kufikisha huduma ya maji safi kwenye kila jimbo lenye uhitaji.
Amesema gharama za jumla kwa visima 10 kwenye majimbo mawili ni takribani sh milioni 760 ambapo kazi ya kuchimba visima na ujenzi wa vituo imekamilika na uwekaji wa miundombinu unaendelea.
Ameongeza pia kazi ya kuweka nishati ya umeme wa jua (sola) kwa ajili ya kusambaza maji imekamilika ambapo kwa kila jimbo vijiji vitano vitakavyofikiwa na mradi vimependekezwa na mbunge wa eneo hilo.

Mhandisi Batakanwa amesema kwa mradi wa kijiji cha Buyagu umebakisha asilimia 10 uweze kukamilika, na hadi kufikia mwishoni mwa mwezi Juni, 2025 utaanza kutoa huduma.
Akizungumza kwa niaba ya wanufaika wa mradi, Mwenyekiti wa kijiji cha Buyagu, Maneno Hassan amekiri mradi huo utaondoa kero ya wananchi kufuata maji safi kwa umbali mrefu zaidi kutoka mkazi yao.

“Kisima hiki kitatupa faida ya maji safi na salama, lakini pia watu watakuwa wanapata maji kwa ukaribu zaidi, kijiji change kina watu zaidi ya 5,000 ambao walikuwa wanafuata maji karibia kilomita tatu.
“Wananchi wa Buyagu niwaombe, mradi huu tuutunze, lakini pia tuchangie gharama ndohgo ambayo imetolewa kwa ajili ya kutunza mradi wetu na kupeleka huduma sehemu nyingine”, amesema Maneno.