Na Clavery Christian – BUKOBA
Waendesha pikipiki mkoani Kagera, wamepatiwa mafunzo ya kutambua abiria wanaobeba dawa za kulevya, ili kuepuka kuhusika na uhalifu wa usafirishaji wa dawa za kulevya, jambalo ambalo linaweza kumsababishia adhabu ya kifungo cha maisha jela.
Akizungumza na waendesha pikipiki wa Manispaa ya Bukoba, Jafari Mtepa kutoka Ofisa ya Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Kanda ya Ziwa amesema bodaboda wanaweza kusaidia kwa kuwatambua mapema abiria wanaojihusisha na biashara hiyo haramu.
Mtepa amesema kuwa njia mojawapo ni kufuata sheria kamili ya kumtaka bodaboda kabla hajampakia mteja kuhakikisha anamuhoji na kujiridhisha shughuli anazofanya sambasamba na kukagua kifurushi au mzigo alioubeba kujua ndani kuna nini ili awe salama.
“Tunatahadhalisha bodaboda kuwa makini na vifurushi wanavyobeba kusafirisha kutoka kwa abiria wao maana adhabu ni kali, kwa mfano ukikutwa na dawa za kulevya kama heroini gramu 200 unafungwa kifungo cha maisha” alisema Mtepa.
Amesema kuwa maeneo maarufu kwa usafirishaji wa dawa za kulevya kwa njia ya pikipiki ni mipakani mwa nchi.
Salvatory Mulangira, ambaye ni Katibu wa Umoja wa Maofisa Usafirishaji maarufu, bodaboda, amesma alikimbizwa na polisi baada ya kudaiwa kupakia abiria aliyebeba dawa za kulevya na walipokamatwa alikuta mteja akiwa amebeba mfuko wa vifaa vya ujenzi kama vile anatoka kazini kumbe ndani ya mfuko huo alikuwa amebeba dawa za kulevya.