Azua Taharuki Baada ya Jeneza Kukutwa Karibu na Makazi Yake

Na William Bundala,Kahama

Katika hali isiyokuwa ya kawaida mkazi mmoja wa Mtaa wa Mwime ya Makungu Kata Mwendakulima Manispaa ya Kahama Mkoani Shinyanga Bwana Kumalija Budeba anayekadiriwa kuwa na umri wa zaidi ya miaka 40 amekutwa na jeneza pembeni ya kichaka cha nyumba yake hali iliyozua taharuki kwa wakazi wa mtaa huo.

Akizungumza na Jambo Fm Kamanda Mkuu wa Sungusungu wa Mtaa wa Mwime Someke John amesema kuwa alipata taarifa za uwepo wa jeneza hilo kutoka kwa vijana waliokuwa wanachunga Ng’ombe katika kichaka hicho na ndipo walipoamua kufika eneo hilo na kuamua kutoa taarifa kwa mtendaji wa kata.

“Nilipata taarifa kutoka kwa vijana waliokuwa wanachunga ng’ombe katika kichaka hicho na ndipo tulipofika na kukuta jeneza hilo ambalo limehifadhiwa kichakani karibu na nyumba ya mzee Kumalija”

Katika hatua nyingine Mke wa mzee huyo Martha Mihambo amesema kuwa jeneza hilo lipo nyumbani kwao tangu mwezi wa saba na mumewe alikuwa analitumia kumtengeneza msanii wa nyimbo za asili aitwae Iddy Masempele ambaye alikuwa anaingia kwenye hilo jeneza ili kuwavutia waangaliaji na baada ya kumaliza mizunguko ya usanii akaliacha katika kichaka hicho.

“Huyu mzee Kumalija alikuwa anamtengezea msanii anaitwa Iddy masempele alikuwa anaingia humo ndani baada ya kumaliza ngoma ndio akaliacha hapa kichakani”amesema Martha.

Awali akizungumza akiwa chini ya ulinzi kwenye Ofisi ya Mtendaji wa Kata ya Mwendakulima Mzee Kumalija Budeba ameiambia Jambo Fm kuwa Jeneza hilo lilikuwa analitumika kwenye sanaa ya ngoma za asili ili kuvuta wateja kupitia msanii Iddy Masempele na kwamba yeye alikuwa hana kazi nyingine ya jeneza hilo na kwamba walikata kibali ofisi ya Utamaduni Manispaa ya Kahama kwa ajili ya kulitumia kwenye shughuli za sanaa.

“Hili jeneza aliliacha Msanii anaitwa Iddy Masempele tulikuwa tunalitumia kwenye ngoma za asili akasahau kulichoma moto,namimi siwezi kuchoma kitu ambacho siyo changu,na tulikata kibali kabisa cha kulitumia jeneza hili” Alisema Kumalija.

Alipotafutwa kwa njia ya simu Afisa Utamaduni Manispaa ya Kahama Felix Tibabala amesema kuwa ofisi yake haijawahi kumkatia mtu yeyote kibali cha kucheza na jeneza na kwamba hakuna ngoma yoyote ya kisukuma inayochezwa kwa kutumia jeneza hivyo mtu huyo achukuliwe hatua za kisheria kama watu wengine.

“Mimi sipo nipo safari ila hakuna mtu yoyote tuliyomkatia kibali cha kucheza na jeneza na Ofisi ya Mkurugenzi Idara ya Utamaduni haiwezi kabisa kutoa kibali cha kutumia jeneza, Jeneza kazi yake ni moja tu kuzikia au kuhifadhia wafu,huyo ni muhalifu kama wahalifu wengine achukuliwe hatua”Alisema Tibabala.

Wakati kila upande ukieleza la kwake kuhusiana na uwepo wa tukio hilo,Kaimu kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Kennedy Mgani,Noemba 25,2024 akizungumza na waandishi wa habari katika Ofisi za Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga ameeleza kwamba  mtu huyo alilipelekea jeneza hilo katika nyumba ya familia na jeshi hilo limebaini kwamba mtu huyo amakabiliwa na msongo wa mawazo kutokana na kutengwa na watu wake wa karibu hali iliyompelekea kukabiliwa na tatizo hilo(Msongo wa Mawazo).

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *