Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anamiringi Macha amewaasa wanafunzi wa Shule ya Wasichana Shinyanga Sekondari kuweka jitihada na nguvu zote katika masomo ili kuhakikisha wanafanya vizuri na baadae waweze kutimiza ndoto na malengo waliyojiwekea.
RC Macha amesema hayo wakati akifanya ukaguzi baada katika shule hiyo akiwa ameambatana na Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga CP Salum Hamduni, ambapo pia ameipongeza manispaa ya Shinyanga kwa usimamizi wa ujenzi wa shule hiyo
“Ninawataka na kuwatia moyo sana ninyi wanafunzi wote katika shule hii, muelekeze bidii na jitihada zenu kubwa katika masomo yenu ili muhakikishe kwamba mnafanya vizuri na mnakuwa mfano wa kuigwa kwa wanafunzi wengine” amesema RC Macha.
Kwa upande wake CP. Hamduni amewataka watumishi wa Serikali mkoani humo kuwa makini katika kutekeleza kazi za Serikali, kutanguliza uzalendo na kuhakikisha kuwa thamani ya fedha inaonekana kwenye kazi zote na hasa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ili iwe na tija iliyokusudiwa.
Aidha Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga Mwl. Alexius Kagunze ameahidi kukamilisha ujenzi wa shule hiyo kwa wakati na kwa viwango vinavyotakiwa na kwamba ujenzi wa shule hiyo unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa Septemba 2024.
Kukamilika ujenzi wa Shule ya Wasichana Shinyanga Sekondari kunatajwa kuwa chachu ya kuwawezesha wanafunzi wa ndani nan je ya Mkoa huo kupata elimu bora kutokana na kuwa na mazingira rafiki, mazuri yenye kuvutia kwa kujisomea pamoja na walimu watakao kidhi mahitaji yao ya kielimu.