Njia za Maambukizi ya Homa ya Ini Na Virusi vya Ukimwi Zinafanana

Wananchi wa Mkoa wa Shinyanga pamoja na maeneo jirani wametakiwa kutembelea vituo vya afya kwa ajili ya kupima afya zao hususani Homa ya Ini, ili kuepukana na changamoto za kiafya ikiwemo kansa ya ini na kifo.

Hayo yamesemwa Septemba 25,2024 na Mratibu wa Kudhibiti UKIMWI, Magonjwa ya Ngono na Homa ya Ini Mkoa wa Shinyanga, Dkt. Peter Mlacha, wakati akitoa elimu ya ugonjwa huo kwa watumishi katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Shinyanga.

Mlacha ameeleza maambukizi ya ugonjwa huo yanasababishwa na virusi ya Homa ya Ini, ikichagizwa zaidi na ngono zembe, kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto pia kwa mfumo wa majimaji (kukumbatiana na mtu mwenye jasho).

“Tujitahidi kufanya vipimo ili kujua hali ya afya zetu, huu ugonjwa namna unavyoambukiza ni sawa na virusi vya UKIMWI, ukishapima na ukagundulika uko salama utapata chanjo na utaishi salama”, amesema Dkt. Mlacha.

Aidha, Dkt.Mlacha amesema takwimu zinaeleza kuwa utafiti uliofanyika, zaidi ya asilimia 95 ya waliopata chanjo ya Homa ya Ini hawajafanikiwa kupata maambukizi ya ugonjwa huo ambao umekuwa na athari kubwa ikiwemo Kansa ya Homa ya Ini.

Vilevile ameainisha baadhi ya athari ambazo zinaweza kumpata mtu mwenye ugonjwa huo ukiachilia Kansa ya Ini, ni ini kutofanya kazi yake, pamoja na kupelekea mtu kupoteza maisha.

Ili kujikinga, Mlacha amewasihi wananchi kuepukana na ngono zembe, kuwa na wapenzi wengi, kufanya ngono salama na muhimu zaidi kupata chanjo mapema kwa ajili ya kuepukana na homa hiyo.

Dkt.Mlacha pia ameeleza rika ambalo linapaswa kupata chanjo mapema zaidi, na ambalo lina hatari kubwa ya kupata maambukizi, ambalo ni kundi la vijana kuanzia umri wa miaka 14 na kuendelea.

Amehitimisha kwa kueleza ugonjwa wa Homa ya Ini hauna TIBA, bali una dawa zinazosaidia kufubaza makali ya virusi hivyo ili visisababishe athari zaidi kiafya.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *