Na William Bundala,Kahama
Wakulima wa zao la Tumbaku Halmashauri ya Ushetu wilayani Kahama Mkoani Shinyanga wameishukuru serikali kufanikisha uaptikanaji wa wanunuzi wengi wa zao hilo msimu huu hali iliyopelekea kuwa na ushindani na kufanikiwa kuuza kwa wakati na wastani mzuri wa bei.
Wakizungumza na Jambo Fm kwa nyakati tofauti wakulima hao wamesema kuwa uwepo wa kampuni nyingi za ununuzi wa tumbaku katika mkoa wa kitumbaku Kahama umewasaidia kuuza tumbaku zao kwa wakati na bei nzuri na kueleza kwamba msimu huu wakitarajia kutapata fedha nyingi kutokana na tumbaku yao kununuliwa kwa bei nzuri.
Wameongeza kuwa katika msimu huu,kampuni za ununuzi wa tumbaku zimewasaidia kutoa elimu kwenye vyama vyao vya ushirika tangu tumbaku ikiwa shambani,wakati wa kuvuna na kuikausha hali iliyopelekea kuuza Tumbaku kwa madaraja ya juu yenye wastani mzuri wa bei.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa chama kikuu cha ushirika (KACU) Tano Nsabi ameipongeza Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu na wizara ya kilimo kwa kuendelea kuwaletea wakulima mbolea ya NPK kwa mfumo wa Ruzuku na kuwataka wakulima kufuata kalenda ya kilimo cha zao hilo.
Sambamba na hayo Nsabi amezipongeza kampuni za ununuzi wa tumbaku kwa kuendelea kununua kwa wastani mzuri wa bei na kutoa wito kwa wajumbe wa vyama vya msingi kuwasimamia wakulima wanapofunga tumbaku ili wasichanganye madaraja na kila upande utende haki na kutimiza wajibu wake.
Mkoa wa kitumbaku Kahama unakadiriwa kuzalisha wastani wa kilo milioni 14 kwa msimu wa kilimo 2023/2024 huku ukiwa na kampuni sita (6) zilizopewa kibali cha kununua zao hilo.