Serikali yakanusha wajawazito kujifungulia chini

Serikali kupitia Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya llemela imetoa ufafanuzi wa taarifa inayosambaa katika mitandao ya kijamii ikionyesha kuwa katika kituo cha Afya cha Buzuruga wakinamama wamekuwa wakipeana zamu ya kujifungulia sakafuni.

Taarifa iliyotolewa leo Disemba 18, 2023 na mkurugenzi wa halmashauri ya manispaa ya Ilemela Wakili Kilomoni Kiburwa Kibamba imesema Awali katika Kituo hicho cha Afya cha Buzuruga kulikuwa na vitanda vitatu kwa ajili ya kujifungulia, na baada ya kuona kumekuwa na ongezeko la wakinamama wanaojifungua Serikali iliongeza idadi ya vitanda vya kujifungulia kutoka vitanda vitatu hadi vitanda sita.

Sambamba na hilo taarifa hiyo imeongeza kuwa Serikali imejenga jengo la mama na moto lenye uwezo wa kulaza wakinamama 42, ambalo liligharimu kiasi cha shilingi Milioni 200 fedha za mapato ya ndani ya Halmashauri, Lengo ikiwa ni kuondoa adha ya wakinamama kulala zaidi ya mmoja katika kitanda kimoja na jengo hilo lilizinduliwa na Mwenge wa Uhuru mwaka 2023 ambalo kwa sasa linatumika.

Kibamba amesema Halmashauri ya Manispaa ya llemela, inauhakikishia umma kuwa katika kituo cha Afya cha Buzuruga, hakuna wakina mama wanaojifungulia chini kama taarifa ya mtandaoni inavyoonyesha.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *