Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye ametoa wito kwa wazazi na walezi nchini kuweka usimamizi wa matumizi ya mitandao ya kijamii kwa watoto.
Akizungumza mkoani Dar es Salaam katika maadhimisho ya miaka 50 ya Chuo cha Ustawi wa Jamii na kilele cha wiki ya Ustawi wa Jamii Waziri Nape amesema watoto wasizuiwe kuitumia mitandao hiyo kwani haikwepeki bali zitumike njia mbadala za kuwaongoza katika matumizi yake.
Amesema wazazi wengi nchini wamewaachia watoto wao kuingia kwenye matumizi ya mitandao ya kijamii bila kuwakinga kwa kutumia njia inayofahamika kama ‘Parental Control’, na kuongeza kuwa kufanya hivyo ni kuiachia mitandao ya kijamii kulea watoto, jambo ambalo matokeo yake ni kuwa na Taifa lisilofaa.
“Wazazi wa Tanzania acheni kuiachia mitandao kuwalea watoto wenu, mtakuwa mnawapeleka kwenye shimo ambalo mtawapoteza, Kwetu sisi ni sawa na kuwatoa kafara watoto”. Amesema Waziri Nape