Wadau wa lishe katika mkoa wa Mwanza wametakiwa kuendelelea kuwahamasisha wazazi katika suala nzima la uchangiaji wa chakula shuleni ili kuboresha ufaulu pamoja na kuongeza maendeleo ya wanafunzi.
Rai hiyo imetolewa na katibu Tawala Mkoa wa Mwanza, Balandya Elikana wakati akifungua kikao cha tathmini ya utekelezaji wa mkataba wa Lishe ngazi ya Mkoa kwa kipindi cha Oktoba – Desemba, 2024 uliowakutanisha wataalamu na wadau mbalimbali wa lishe.

Amesema, Mei na Juni uhamasishaji utafanyika katika Wilaya za Ukerewe na Magu na ameziagiza shule kuwa na maeneo kwa ajili ya kilimo kwa lengo la kuzalisha mazao yao wenyewe.
“Tutajigawa ili twende kwenye baadhi ya maeneo kuhamasisha upatikanaji wa chakula mashuleni,” amesema ndugu Balandya.

Awali, Mganga Mkuu wa Mkoa, Dkt. Jesca Lebba ameeleza kuwa suala la wanafunzi kupata chakula chenye lishe ni suala muhimu sana kwa kila mwanafunzi na ametoa wito kwa wazazi kushirikiana na serikali kufanikisha upatikanaji wa vyakula shuleni.
Katika hatua nyingine Lebba pia ametoa ushauri kwa halmashauri zote za mkoa huo kupanga bajeti na kuitekeleza ili kuwezesha watoto wa shule kupata chakula wakati wa masomo na kushirikiana na wadau.

Kwa upande wa wadau hao wa lishe katika mkoa wa Mwanza wameshauri Kamati ya Lishe Mkoa kufanya juhudi za binafsi kutafilia na kuwekea mkazo na nguvu katika swala la kutungwa kwa sheria kwa wazazi na walezi wa wanafunzi ambao hawachangii chakula shuleni ili kuweza kuongeza upatikanaji wa chakula mashuleni.
