Na Eunice Kanumba – Shinyanga.
Wafanyabiashara ndogondogo katika Manispaa ya Shinyanga, wametakiwa kuchangamkia fursa ya mikopo ya silimia 7 yenye riba ndogo inayotolewa na Serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wanawake na Makundi Maalumu ili kuwasidia kuinuka kiuchumi na kuwa wafanyabiashra wa kati.
Wito huo umetolewa Mei 14, 2025, na Afisa wa Wizara hiyo, Ezekiel Philipo kutoka Kitengo cha Makundi Maalumu, katika kikao cha utoaji wa elimu kuhusu usajili na utambuzi wa wafanyabiashara ili waweze kupata vitambulisho vinavyowaruhusu kufaidika na mikopo hiyo kilichofanyika leo katika soko la mitumba lililopo kata ya Ngokolo halimashauri ya manispaa ya Shinyanga.

Amesema, ili kupata mikopo hiyo ni lazima Wafanyabiashara hao wasajiliwe na kutambuliwa kwenye mifumo, ili wapate vitambulisho ambavyo vitawasaidia kupata mikopo katika Benki ya NMB, huku pia wakitakiwa kufungua akaunti za biashara katika benki hiyo, ili waweze kuwekewa fedha kwa mfumo wa kibenki kwenye Akaunti zao.
“Tumefika Shinyanga kutoa elimu kwa wafanyabiashara ndogo ili wachangamkie mikopo ya serikali isiyo na dhamana, yenye riba nafuu ya asilimia 7. sharti pekee ni kuwa na kitambulisho kinachopatikana baada ya usajili rasmi,” alisema Philipo.

Aidha, amesema mara baada ya kutoa elimu hiyo ya kujisajili na kutambuliwa,kwamba wanategemea kuona idadi kubwa ya wafanyabiashara katika Manispaa ya Shinyanga wanaongezeka kupata mikopo hiyo sababu idadi bado ipo chini.
Kwa upande wake, Afisa Maendeleo ya Jamii Mwandamizi Kitengo cha Makundi Maalumu kutoka Wizara hiyo, David Malebetho amewataka Wafanyabiashara hao kujitokeza kwa wingi kusajiliwa, hatua ambayo itawasaidia kupata mikopo na kuiwezesha serikali kupata takwimu zao sahihi kwa ajili ya kupanga maendeleo kikamilifu.

Naye Mratibu wa zoezi la usajili na utambuzi wa Wafanyabiashara ndogo ambaye pia ni Afisa Biashara Mkoa wa Shinyanga, Rose Tungu amesema bado kuna mwitikio mdogo wa kuchangamkia mikopo hiyo, licha ya kuwa na masharti na riba nafuu.
“Serikali imeanzisha mikopo hii ili kuinua uchumi wa wafanyabiashara ndogo, lakini mwamko wa kuchukua mikopo bado ni mdogo hapa Shinyanga,” amesema Rose Tungu.

Kwa upande wake Afisa kutoka Benki ya NMB Tawi la Manonga Manispaa ya Shinyanga, Albini Mpona ametaja idadi ya Wafanyabiashara ndogo ambao mpaka sasa wamechangamkia mikopo hiyo na kupata pesa kuwa ni 15 pekee na kudai kuwa mikopo hiyo inatolewa kuanzia sh.100,000 hadi Milioni 4 na hakuna dhamana.
Baadhi ya wafanyabiashara walioshiriki katika mafunzo wameeleza kufurahishwa na elimu waliyopewa, huku wakiahidi kujisajili ili kufaidika na mikopo hiyo ya serikali, na kuondokana na mikopo yenye masharti magumu kutoka taasisi zisizo rasmi.

Jumla ya shilingi million 21 na laki Tisa zimeshakopeshwa kwa Wafanyabiashara ndogondogo katika Manispaa ya Shinyanga, kati ya shilingi million 140 zimetolewa na Serikali kufanikisha zoezi hilo katika manispaa ya Shinyanga