Na Pascal Tuliano, Tabora.
Jamii imeaswa kuweka mkazo katika Suala la malezi bora kwa watoto ili kujenga familia yenye maadili katika jamii.
Rai hiyo imetolewa Na kaimu katibu tawala wa Mkoa wa Tabora, Mhandisi Faustin Turai katika kongamano la maadhimusho ya siku ya kimataifa ya familia iliyoadhimishwa kimkoa katika ukumbi wa Mwanakiyungi uliopo manispaa ya Tabora.

Akimuwakilisha katibu tawala wa mkoa huo, mhandisi Turai amesema familia bora ni nguzo muhimu ya kimaendeleo katika taifa letu.
“Sisi kama wanafamilia tunalo jukumu kubwa la kuhakikisha watoto wetu tunawalea katika mazingira yaliyo bora, ili kujenga taifa lililo bora pia.”

Ameongeza kuwa kulingana na mazingira ya sasa ni vyema wazazi kuwa makini na watoto wao dhidi ya vitendo vya ukatili ikiwemo ulawiti.
“Nitoe rai kwa wazazi kuongeza usimamizi wa watoto dhidi ya ukatili na ulawiti, na kutoa taarifa katika mamlaka husika pindi mnapobaini viashiria vya ukatili kwa watoto wenu.”

Nao baadhi ya wajumbe na washiriki wa kongamano Hilo wameiomba serikali kuweka mikakati madhubuti inayolinda usalama wa watoto hasa katika mitandao ya kijamii.
Maadhimisho ya siku ya familia duniani huadhimishwa Kila mwaka ifikapo Mei 15, na mwaka huu yamefanyika kitaifa mkoani Mwanza.