HUDUMA ZA MACHO: SERIKALI YAWAONYA WAMILIKI WA MADUKA YA DAWA

Serikali Nchini, imewaonya Wamiliki wa Maduka ya Dawa kuacha kufanya biashara ya huduma za macho kama lenzi tiba na fremu za miwani kwani ni kwenda kinyume na Sheria ya Optometria Sura ya 23.

Wito huo umetolewa na Msajili Baraza la Optometria, Sebastiano Millanzi na Msajili Baraza la Famasi, Beatus Mpogoza Februari 20, 2025 jijini Mwanza kufuatia ukaguzi ulifanyika kwa pamoja na kubaini baadhi ya wamiliki na watoa dawa ambao wachanganya bidhaa hizo ambazo kimsingi zinatakiwa kusimamiwa na Baraza la Optometria nchini.

Akizungumza katika duka la dawa la Jeda Pharmacy liliopo Mtaa wa Uhuru, mara baada ya kukuta zaidi ya lenzi 1,560 zikiwa katika makasha 52, Msajili Baraza la Optometria, Millanzi amesema bidhaa za optometria kwa mujibu kifungu cha 40 (1)(a) na (b) cha Sheria ya Optometria Sura ya 23 imeweka wazi kuwa ni marufuku mtu yeyote kufanya biashara ya vifaa au huduma za Optometria bila kutajwa kwenye Sheria hii.

“Nimeendelea kusisitiza kwa sasa tupo kwenye usimamizi shirikishi ambao hatutaki kumuonea mtu bali kumuelimisha kisha afuate taratibu ikiwa ni pamoja na kusajili kituo na kuajiri mtaalam wa Optometria atakayesimamia shughuli zote za huduma za optometria,” amesema.

Ameongeza kuwa, Baraza linatoa miezi mitatu ili mhusika aweze kufuata taratibu za kusajili kituo na bidhaa zote zilizokutwa dukani hapo zitakuwa chini ya uangalizi wa Ofisi ya Mganga Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana hadi pale mhusika atakapokamilisha taratibu hizo.

Naye Msajili wa Baraza Famasi kupitia Mkuu wa Ofisi ya kanda ya Ziwa inayohusisha mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Geita, Mara, Simiyu na Kagera, Mfamasia Beatus Mpogoza amesema kwa mujibu wa Sheria za Famasia hairuhusiwi kwa mtaalam wa Famasi kuuza lenzi wala fremu za miwani na kufanya hivyo ni kwenda kinyume na Sheria ya Famasia ya Mwaka 2011.

“Sisi tutamtaka Mtaalama huyu ambaye amesajiliwa chini ya Baraza la Famasi kutoa maelezo ya kina ni kwa nini amejihusisha na uuzaji wa lenzi jambo ambalo ni kinyume na matakwa ya Sheria yetu ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa,” amesema Mpogoza.

Msajili Baraza la Optometria na jopo lake wapo kwenye usimamizi shirikishi mkoani Mwanza ambapo pamoja na mambo mengine wanatoa elimu kwa wamiliki wa vituo vinavyotoa huduma za optometria zikiwemo hospitali, kliniki za macho, kliniki za Optometria na vituo vinavyouza na kusambaza fremu za miwani na lenzi tiba.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *