Categories

Do you have a Story?

Call us on 0677 644 444 to submit your news story or incident report!

Upinzani Nchini Msumbiji Waandamana Kupinga Matokeo Ya Uchaguzi

Chanzo: Dw

Vikosi vya usalama nchini Msumbiji vimefyatua risasi kutawanya mamia ya wafuasi wa mgombea wa upinzani Venancio Mondlane, kulingana na video zilizosambaa mitandaoni na Mondlane ambaye anadai kushinda uchaguzi wa rais uliofanyika wiki iliyopita.


Mgombea huyo wa upinzani amedai kuwa vijana watatu wamejeruhiwa kwa risasi za moto, na kwamba mmoja wao yuko katika hali mbaya sana kwani alipigwa risasi miguu yote miwili.


Akizungumza na waandishi wa habari, Msemaji wa polisi Gilberto Inguane hakuthibitisha uwepo wa majeruhi yeyote ila amesema kwamba polisi walitumia mbinu za kuwatawanya baada ya waandamanaji kuwarushia mawe na kuchoma matairi na kufanikiwa kuwakamata watu wanne.


Mondlane na mamia ya wafuasi waliandamana katika mji wa kaskazini-mashariki wa Nampula, kupinga tangazo la mamlaka ya uchaguzi lililotolewa Jumatatu kwamba chama tawala cha Frelimo kilishinda uchaguzi wa Oktoba 9 katika jimbo hilo kwa asilimia 66.


Nchi hiyo ilifanya uchaguzi wa rais, bunge na magavana wa majimbo huku chama tawala cha Frelimo kikitarajiwa kushinda kikiwa kimetawala nchi hiyo tangu ilipopata uhuru kutoka kwa Ureno miaka 49 iliyopita.

Itakumbukwa kuwa Mondlane, akiwa na uungwaji mkono na chama kidogo cha Podemos, alidai ushindi mara tu baada ya siku ya kupiga kura na sasa ameitisha mgomo wa nchi nzima dhidi ya kile anachodai kuwa ni udanganyifu mkubwa.


Hata hivyo Mwanasheria mkuu wa Msumbiji alimuonya Mondlane siku ya Jumanne kwamba kudai ushindi kabla ya matokeo rasmi kutangazwa kunaweza kuchochea machafuko ya kijamii na ni kinyume cha katiba.


Kulingana na takwimu za Mondlane, alizochapisha kwenye mitandao ya kijamii, anadai kupata asilimia 53 ya kura katika uchaguzi wa urais kufikia siku ya Jumanne, huku asilimia 67 ya kura zikiwa zimehesabiwa, dhidi ya asilimia 36 za mgombea wa Frelimo Daniel Chapo.


Matokeo rasmi ya nchi nzima yanatarajiwa kutangazwa Oktoba 24, 2024.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *