Wakulima Toeni Ushirikiano kwa Bodi

Na William Bundala,Kahama

Wakulima wa zao la Pamba na Tumbaku wilayani Kahama Mkoani Shinyanga wametakiwa kutoa ushirikiano kwa bodi mpya iliyochaguliwa ya chama kikuu cha ushirika (KACU) ili kuboresha utendaji kazi,kuinua na kukiendeleza chama hicho cha wakulima.

Wito huo umetolewa leo na mwenyekiti mpya wa chama kikuu cha ushirika (KACU) Emmanuel Nyambi wakati akikabidhiwa ofisi na kaimu mwenyekiti wa chama hicho aliyemaliza muda wake Tano Nsabi.

Nyambi amesema kuwa maendeleo ya Chama cha wakulima Kahama yataletwa na wajumbe wa bodi kwa kushirikiana na wakulima wenyewe na kuwaomba wakulima wawaunge mkono pamoja na wajumbe wa bodi kumpa ushirikiano kwakuwa bodi iliyoingia madarakani ndiyo iliyofanya maendeleo yote ya awali katika chama kikuu cha KACU.

Kaimu Mwenyekiti wa chama kikuu cha KACU Tano Nsabi (Kulia) akimkabidhi nyaraka Muhimu za Chama Mwenyekiti Mpya Bwan Emmanuel Nyambi (Kushoto).

Kwa upande wake kaimu mwenyekiti wa KACU aliyemaliza muda wake Tano Nsabi amesema kuwa amekabidhi ofisi ikiwa salama na kuiomba bodi iliyoingia madaraka chini ya Mwenyekiti Emmanuel Nyambi kutenda kazi kwa uadilifu kwa kuwa Chama kikuu cha KACU kinategemewa na watu wengi na kuwaomba wakulima kutoa ushirikiano kwa bodi mpya iliyopo madarakani.

Nao baadhi ya wajumbe wa KACU Ngambanila Bundala na Lameck Machelewa wamesema kuwa wataendelea kufanya kazi kwa ushirikiano ili kukiinua chama kikuu cha KACU pamoja na kutafuta fursa mbalimbali zitakazosaidia kuwainua wakulima.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *