Na Melkizedeck Antony,Mwanza
Binti Akwelina Martin (17) aliyekuwa mkazi wa Nyamanoro wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza amefariki dunia huku mwili wake ukiwa nusu uchi ukiwa umetupwa uchochoroni.
Akielezea tukio hilo mbele ya waandishi wa habari Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Mwanza DCP Wilbroad Mutafungwa amesema tukio hilo lilitokea siku ya tarehe Mei 27,2024 majira ya saa 12 alfajiri huko katika mtaa wa Nyamanoro Mashariki Wilaya ya Ilemela Mkoa wa Mwanza ambapo jeshi la polisi ndani ya mkoa huo lilipata taarifa kwamba mwili wa binti huyo umetupwa uchochoroni ambapo baada ya kuukagua ulikutwa ukiwa na michubuko katika sehemu za mgongoni na kwenye mkono wa kushoto.
Baada ya ukaguzi wa awali mwili huo ulipelekwa katika hospitali ya rufaa mkoa wa Mwanza Sekou Toure ambapo baada ya kufanyiwa uchunguzi ilibainika kua binti huyo aliuawa huku pia ukiwa na dalili zilizoonesha kuwa binti huyo aliingiliwa kimwili.
Kufuatia kutokea kwa tukio hilo,Jeshi la Polisi mkoa wa Mwanza linawashikilia watu Wawili ambao ni Jovin Kamando (26) mkazi wa kilimahewa pamoja na Kelvini Raymond (27) mkazi wa Kitangiri ambao inadaiwa kuwa wate walikuwa na uhusiano wa kimapenzi na marehemu.
Taarifa za awali za tukio hilo zinaonyesha chanzo cha kifo cha binti huyo ni wivu wa kimapenzi na uchunguzi bado unaendelea na utakapokamilika watuhumiwa watafikishwa Mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria.
Wakati huo huo,Jeshi la polisi mkoani Mwanza linawashikilia watu sita kwa kosa la kumuua mama yao mzazi aliyefahamika kwa jina la Shija Magelanya (77) wakimtuhumu kuwaroga wajukuu zake na kuwasababishia ukichaa.
Akizungumzia tukio hilo Kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Mwanza DCP Wilbrod Mutafungwa amesema tukio hilo lilitokea siku ya tarehe moja ya mwezi huu majira ya saa mbili na nusu usiku huko katika kijiji cha Nduwa kata ya Kasororo wilaya ya Misungwi ambapo bibi huyo wakati akiwa amekaa na wajukuu zake wakila chakula ghafla walivamiwa na mwanaume mmoja aliyekuwa na panga kisha akaanza kumkata maeneo ya kichwani na mabegani na kupelekea kupoteza maisha hapo hapo.