Mvua zinazoendelea kunyesha maeneo mbalimbali nchini zimekata mawasiliano katika madaraja ya Mto Msadya pamoja na Daraja la Mto kibaoni katika Jimbo la Kavuu lililopo katika Halmashauri ya Mpimbwe Wilaya ya Mlele Mkoa wa Katavi.
Mvua hizo zilizonyesha usiku wa kuamkia Aprili 14, 2024 zimesababisha adha kwa magari na wananchi wanaotumia daraja hilo hususani katika vitongoji vya Ikuba, Usenga na Igongo,
kwa Daraja la Kibaon, mawasiliano baina ya Kibaoni na Usevya katika halmashauri hiyo ya Mpimbwe yamekatika na kusababisha njia kufungwa kutokana na maji kuvunja daraja hilo.
Mbunge wa jimbo la Kavuu na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendekeo ya Makazi, Geophrey Pinda akiwa na viongozi wa Serikali na Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Mlele wamefika maeneo yaliyoathirika kwa lengo la kujionea uharibifu na athari iliyopapatikana kwa wananchi na kuwapa pole wote walioathirika na mafuriko hayo huku akiwataka wananchi hususani vijana wanaoishi eneo la Mto Msadya kuanza kuchukua hatua za uhifadhi mazingira.
Mkuu wa Wilaya ya Mlele mkoani Katavi Alhaji Majid Mwanga ametaka kuwepo kwa tahadhari kwenye maeneo yote yaliyoathirika huku akiwataka watendaji wa kijiji na kata kuzunguka na kupata taarifa ya maeneo yaliyoathirika kwa kushirikiana na ofisi ya halmashauri ya Mpimbwe ili wilaya ichukue hatua stahiki.
Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Mpimbwe Shamim Daud Mwariko kwa upande wake amewataka wananchi wanaoishi maeneo yaliyoathirika kutopita katika njia zisizoruhusiwa kwa kuwa ni vigumu kufahamu muda gani maji yatajaa.