ZAIDI YA MIL. 890 KUTUMIKA KATIKA UJENZI WA MADARASA 25 CHATO

Na Gideon Gregory – Dodoma.

Serikali imepanga kutumia kiasi cha shilingi Milioni 890.3 katika mwaka wa fedha 2025/2026, kwa ajili ya ujenzi wa madarasa 25 na matundu ya vyoo 75 katika shule kongwe za Bukiriguru, Busaka, Buzirayombo, Ihanga, Katete, Kibumba, Kinsabe, Katende, Kitela, Mwabasabi, Minkoto, Mwangaza, Nyakato, Nyamirembe na Nyanghomango katika Wilaya ya Chato.

Hayo yamebainishwa leo Aprili 10, 2025 Bungeni Jijini Dodoma na Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Zainabu Katimba wakati akijibu swali Dkt. Medard Kalemani, Mbunge wa Chato aliyehoji ni lini Serikali itakarabati Shule kongwe za Msingi katika Jimbo la Chato.

“Mwaka 2024/2025, Serikali imetenga shilingi milioni 476.2 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa 10 na matundu ya vyoo 77 katika shule kongwe za Bwanga, Bwina, Busalala, Ilemela, Itanga, Katale, Katende, Mwangaza, Nyantimba, Nyarutembo na Nyisanzi zilizopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Chato,”amesema. 

Aidha, ameongeza kuwa Serikali itaendelea kuboresha shule kongwe za msingi zikiwemo za Halmashauri ya Chato kadiri ya upatikanaji wa fedha.

Akijibu swali la nyongeza la Mbunge huyi juu ya lini fedha hizo zitatoka, Katimba amemuhakikishia kuwa fedha hizo kiasi cha shilingi Milioni 890.3 zitafika kwaajili kwa wakati ili kuhakikisha zinakarabati shule hizo kongwe.

“Lakini nitumie nafasi hii kuendelea kutoa msisitizo kwa Mkurugenzi wa Halmashauri kuhakikisha anaendelea kuzifanyia tathmini shule kongwe hizi 169 katika Jimbo la Mheshimiwa Mbunge na kuziweka katika mpango na bajeti kwaajili ya kuendelea kuzikarabati ili shule hizi ziweze kuwa katika hali nzuri na ziweze kuwanufaisha wanafunzi wetu,” amesema. 

Leo Bunge limeanza kujadili Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026. 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *