Mstahiki Meya wa Manispaa ya Songea, Michael Mbano ametoa wito kwa familia zote kushiriki kikamilifu katika uchangiaji wa damu kwa hiari.
Ametoa kauli hiyo leo katika kilele cha maadhimisho ya Wiki ya Mchangia Damu Kitaifa yaliyofanyika katika viwanja vya Bustani ya Manispaa ya Songea, mkoani Ruvuma.
Wiki hiyo ilianza rasmi tarehe 01 Juni 2025 na kufikia tamati leo, tarehe 14 Juni 2025, sambamba na Siku ya Wachangiaji Damu Duniani inayoadhimishwa kila mwaka tarehe hiyo.

Akizungumza kwa niaba ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma, Mbano alieleza kuwa kuchangia damu ni hatua muhimu ya kuokoa maisha, hasa katika nyakati za dharura. Alisisitiza kuwa jukumu hilo linapaswa kuchukuliwa kwa uzito na kila familia.
Kwa mujibu wa takwimu za Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, Mkoa wa Ruvuma una idadi ya watu takribani milioni 1.8. Mahitaji ya damu kwa mwaka ni chupa 14,789, lakini mwaka 2024 mkoa uliweza kukusanya chupa 7,016 pekee, sawa na asilimia 47 ya mahitaji.
Kwa kipindi cha Januari hadi 12 Juni 2025, jumla ya chupa 4,040 za damu zilikusanywa, ambazo ni asilimia 27 ya lengo la mwaka huu.

Aidha, Mbano alibainisha kuwa watumiaji wakubwa wa damu salama
Watoto chini ya miaka 5 asilimia 50
Mama wajawazito asilimia 30 Wahanga wa ajali, wagonjwa wa ndani na wanaofanyiwa upasuaji asilimia 20
Kwa upande wake, Mganga Mkuu Msaidizi wa Mkoa wa Ruvuma, Dkt. Chihoma Mhako, alieleza kuwa damu haiwezi kutengenezwa viwandani wala kuuzwa madukani, hivyo jamii inapaswa kuelewa umuhimu wa kuchangia damu kwa hiari.
Dkt. Mhako aliongeza kuwa katika wiki ya mchangia damu pekee, jumla ya chupa 1,213 zilikusanywa, sawa na asilimia 117.16 ya lengo la wiki hiyo, ambalo lilikuwa chupa 1,035.