Categories

Do you have a Story?

Call us on 0677 644 444 to submit your news story or incident report!

Waziri Mavunde Akabidhi Magari 25 Kwa Tume Ya Madini

Na Gideon Gregory, Dodoma.

Waziri wa Madini Anthony Mavunde amekabidhi jumla ya magari 25 kwa Tume ya Madini ili kuboresha utendaji kazi na kuongeza ukusanyaji wa maduhuri huku akitoa rai kwa watumishi watakaokadhiwa magari hayo kuhakikisha wanayatumia ipasavyo ili kuweza kufikia lengo lililokusudiwa.


Waziri Mavunde ameyasema hayo jijini Dodoma wakati wa hafla ya uzinduzi wa magari hayo na kuongeza kuwa jumla ya fedha kiasi cha shilingi Bilioni 18 zimetengwa kwa ajili ya ununuzi wa magari na pikipiki.


Amesema katika mwaka huu wa fedha Wizara ya Madini imepangiwa kukusanya shilingi trilioni moja hivyo vitendea kazi hivyo vitasaidia katika kufikia lengo.


“Magari haya 25 yanaenda kuongeza kasi ya ukusanyaji wa mapato katika mikoa ya kimadini na katika mwaka huu wa fedha katika kipindi cha siku 90 tumekusanya shilingi bilioni 287 ikiwa tumevuka lengo la kukusanya shilingi bilioni 241 katika kipindi tajwa,”amesema Mavunde


Ameongeza kuwa bajeti ya wizara ya madini imeongezeka kutoka shilingi bilioni 89 mwaka 2016 hadi kufikia shilingi bilioni 231 mwaka huu.


“Jukumu tulilonalo ni kuhakikisha sekta hii ya madini inatoa mchango chanya katika ustawi wa uchumi wa Taifa kwa kuhakikisha tunaongeza kiwango cha makusanyo”.amesema Mavunde


Katika hatua nyingine Mavunde amesisitiza kuwa magari hayo yatafungwa vifaa maalumu vya kuyafuatilia ili yasitumike vibaya.


Kwa upande wake Kaimu Mtendaji Mkuu wa Tume ya Madini Mhandisi Ramadhani Lwamo amesema serikali imekuwa ikiongeza bajeti kwa wizara ili kuhakikisha kunakuwa na vitendea kazi vya kutosha huku akifafanua kuwa vifaa hivyo vitasaidia kuongeza kasi ya ukusanyi mapato ili kuongeza makusanyo ya serikali.


Kwa upande wake Ofisa Madini Mkazi wa Mererani Nchangwa Marwa ameipongeza serikali ya Awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya kuboresha utendaji kazi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *