Chanzo:BBC
Jumla ya Maseneta 49 wamepiga kura ya kumuondoa madarakani aliyekuwa Naibu Rais wa Kenya Rigathi Gachagua kwa ukiukwaji wa katiba ya nchi hiyo.
Mwanasiasa huyo alikuwa akikabiliwa na mashitaka 11, huku akishindwa kutokea na kujitetea mbele ya Bunge la Seneti siku ya oktoba 17.
Kulingana na katiba ya Kenya, Naibu Rais anafikia kikomo cha nafasi hiyo baada ya kuondolewa na Bunge la Taifa na Bunge la Seneti la nchi hiyo.
Hata Hivyo Rais William Ruto tayari amemteua Waziri wa Usalama wa Ndani Kithure Kindiki kuwa Naibu Rais ajaye ili kuziba nafsi ya Gachagua
Jina la Kindiki limewasilishwa Bungeni ambapo Wabunge wanatarajiwa kulipigia kura ndani ya siku 60 baada ya kupokea jina hilo.
Katiba inasema pindi Rais anapowasilisha uteuzi kwenye Bunge, Wabunge watapiga kura ya kulikataa au kuliidhinisha jina hilo na hakuna sharti la kura ya thuluthi mbili.
Prof. Kindiki, ambaye kwa sasa anahudumu kama Waziri wa Mambo ya Ndani na Utawala wa Kitaifa, atahitaji idhini kutoka kwa Bunge la Kitaifa kabla ya kushika nafasi ya Naibu Rais.
Katika maandalizi ya uchaguzi mkuu wa 2022, Kindiki alikuwa miongoni mwa waliopendekezwa kuwa mgombea mwenza wa Ruto lakini hatimaye akaamua kumchagua Gachagua kwa sababu ya umri wake na alifikiri wangeelewana zaidi.