MKUU wa Mkoa wa Katavi Mwanamvua Mrindoko, ameitaka jamii kurejea kwenye misingi ya malezi bora ya watoto na vijana, akieleza kuwa jamii ya sasa imezembea katika kuwalea watoto kwa maadili, ujasiri na uwajibikaji.
Mrindoko amesema hayo wakati wa misa maalum ya kuombea amani iliyoandaliwa na Umoja wa Wanawake Wakatoliki Tanzania (WAWATA), katika Kanisa la Kristu Mfalme, Parokia ya Kanoge, Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo.

Katika hotuba yake, Mrindoko ameonesha kusikitishwa na namna baadhi ya wazazi na walezi walivyopoteza mwelekeo wa malezi ya kizazi kipya, akisisitiza umuhimu wa kurejea kwenye maadili mema na mafundisho ya msingi ambayo yamejenga jamii imara kwa miaka mingi.
“Tumezembea sana kwenye suala la malezi,niombe sasa turejee kwenye wajibu wetu, kwa namna tulivyolelewa sisi watu wa umri wa kati, ni jukumu letu kuhakikisha watoto wetu na vijana wetu wanajimudu kimaisha”.

Ameongeza kuwa, “Tuwafundishe maisha, tuwafundishe kujitegemea, kuwajibika kwa familia zao na kwa taifa kwa ujumla,tukifanya hivyo tutakuwa tumeponya sana, lakini tukiamua kupotezea na kuendeleza tamaduni zisizo za kwetu, na kuwalea watoto kama mayai, tutatengeneza kizazi kibaya sana chenye udhaifu wa kimaadili na kiuchumi”.
Pamoja na wito huo wa malezi, Mrindoko amewahamasisha wananchi kujitokeza kushiriki kikamilifu katika Uchaguzi Mkuu ujao, akiwataka wapiga kura waliopo kuhakikisha wanatunza kadi zao za kupigia kura, na kwa wale ambao hawana, kujitahidi kujitokeza kujiandikisha.

“Kura yako ni sauti yako, tushiriki kwa amani, heshima na umoja ili kuendeleza demokrasia na kuchagua viongozi wenye dira na maono kwa ajili ya maendeleo ya taifa letu,” amesisitiza.
Kwa upande wao waamini wa dini mbalimbali walipata fursa ya kutoa mafundisho na maombi mbalimbali huku wakiendelea kusisitiza suala la upendo,amani na mshikamano kwa wananchi wote pasipokujali dini,itikadi wala makabila.

Tukio hilo limehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali, waamini wa dini ya Kiislam, waamini wa madhehebu mbalimbali ya kikristo pamoja na waamini wa Kanisa Katoliki waliokusanyika kwa ajili ya kuliombea amani Taifa kuelekea uchaguzi na mustakabali wa maendeleo ya Mkoa wa Katavi.