
Jeshi la polisi katika mkoa wa Mwanza linawashikilia watu 35 kwa tuhuma za kuhifadhi mafuta ya dizeli na petrol katika makazi yao bila kufuata utaratibu huku pia wakijihusisha na uuzaji wa mafuta hayo bila kua na kibali.
Akizungumza na waandishi wa habari kamanda wa polisi mkoa wa Mwanza DCP Wilbrod Mutafungwa amesema watu hao wamekamatwa katika kata za Koromoje, Ngula, Ilemela, Nyashishi, Buhongwa kupitia msako maalum ulioanza april 30 hadi may 31 mwaka huu.
Kamanda Mutafungwa amesema watuhumiwa hao wamekutwa na mafuta ya dizeli lita 685, betri mbili za magari, pikipiki moja, mapipa mawili mipira kumi ya kunyonyea mafuta, madumu 85 pamoja na vitu vingine vyenye thamani ya shilingi milioni nne.
“Vielelezo vilivyokamatwa ni mafuta ya Diesel lita 685, Betri 2 za gari, Pikipiki 1 aina ya SANLG yenye namba za usajili MC711 DJM, Earthroad 2, Pipa 2, mipira 10 ya kunyonyea mafuta, Madumu 85 yanayotumika kufanyia uhalifu, Waya wa fensi bando 1, vyote vikiwa na thamani ya shilingi milioni nne laki nne na sitini na tatu mitisa na kumu”
Aidha Mutafungwa pia amesema watuhumiwa 21 wamehojiwa na kufikishwa mahakamani na watuhumiwa 14 watafikishwa mahakani baada ya upelelezi ukamilika.
Katika tukio lingine jeshi la polisi katika mkoa huo linawashikilia watu wawili ambao ni Jeny Odhiambo na Samora Nyandimo kwa kukuta wakiwa wanasafirisha madawa ya kulevya aina ya bangi kilogramu 194 walikuwa wakitoka nayo Tarime mkoani Mara kuja Mwanza.
“Jeshi la polisi lilifanikiwa kuwakamata Jane Joseph Odhiambo, miaka 53, mkulima na mkazi wa Tarime, mkoa wa Mara na Samora Osewe Nyadimo, miaka 47, mkulima na mkazi wa Pansiasi, wilaya ya Ilemela, wakiwa wanasafirisha Bhangi kilogramu 194.1 wakitokea Tarime kuja mkoa Mwanza wakitumia gari yenye namba za usajili T668 DMY mali ya Jane Joseph Odhiambo, watuhumiwa wote wamehojiwa na watafikishwa mahakani baada ya upelelezi kukamilika”
Kufuatia matukio hayo jeshi la polisi katika mkoa wa Mwaza limetoa wito kwa wananchi wa mkoa huo kuacha kujihusiha na vitendo ambavyo vipo kinyume na sheria za nchi huku pia wakijiepusha na vitendo vya kiuhalifu kwani jeshi hilo halitasita kuwachukulia hatua wale wote watakaokwenda kinyume na sheria hizo.