Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) imepokea tuzo ya heshima ya utunzaji wa mazingira katika maadhimisho ya kilele cha Siku ya Mazingira Duniani yaliyofanyika jijini Dodoma.
Tuzo hiyo imetolewa kutokana na mafanikio ya PPRA katika kubuni na kutekeleza mfumo wa kielektroniki wa ununuzi wa umma uitwao NeST, ambao umewezesha kuondoa matumizi ya karatasi katika shughuli za ununuzi wa serikali.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kupokea tuzo hiyo, Meneja wa Mradi wa NeST, Bw. Michael Moshiro, amesema kuwa mfumo huo umeleta mageuzi makubwa katika sekta ya ununuzi kwa kusaidia serikali kupunguza matumizi ya rasilimali zisizohitajika, hasa karatasi.
Ameeleza kuwa kupitia NeST, mchakato mzima wa manunuzi sasa unafanyika kidijitali, jambo linalochangia moja kwa moja katika kulinda mazingira.

Moshiro amesisitiza kuwa matumizi ya mfumo huo yameiwezesha serikali kuokoa fedha nyingi ambazo hapo awali zilitumika kununua karatasi na vifaa vingine vinavyohusiana.
Fedha hizo sasa zimeelekezwa kwenye utekelezaji wa miradi mingine ya maendeleo kama afya, elimu, na miundombinu, hivyo kuongeza tija katika matumizi ya rasilimali za umma.

Aidha, NeST imeongeza uwazi na ufanisi katika michakato ya manunuzi, huku ikirahisisha ufuatiliaji wa taarifa na kumbukumbu kwa njia ya kielektroniki.