WANASIASA ACHENI KUTUMIA VIKUNDI VYA MIKOPO KWA MASLAHI YENU BINAFSI-RC MACHA.

 NA EUNICE KANUMBA 

 Viongozi wa Serikali na Wanasiasa wameonywa kuacha tabia ya kuvitumia vikundi vinavyopewa mikopo ya asilimia kumi na Halmashauri kujinufaisha wenyewe kwa kuingilia majukumu yao na kushindwa kufikia lengo la serikali kusaidia wananchi.

Hayo yameelezwa na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mh. Anamringi Macha leo wakati wa ziara yake ya kufuatilia kilimo cha zao la pamba na utoaji wa mikopo kwa vikundi vya wanawake,vijana na walemavu.

Mkuu wa Mkoa amesema serikali inatoa fedha hizo kwa wananchi ili kuwawezesha kujikwamuwa kiuchumi kwa kufanya shughuli ambazo zitachangia kuongeza kipato chao  ikiwa ni pamoja na kufanya shughuli za kilimo,ufugaji na miradi mingine ambayo inaweza kuwapatia kipato kikubwa.

Amesema wapo baadhi ya watumishi wa umma wanajinufaisha na mikopo hiyo jambo ambalo ni kinyume na utaratibu na kuzitaka Halmashauri kuhakikisha wanatoa elimu kwa vikundi vyote vilivyokidhi vigezo vya kupata mkopo ili kuepuka changamoto ya kushindwa kurejesha mikopo kwa wakati.

“Kuna baadhi ya viongozi walikuwa na vikundi vyao vya mfukoni ambavyo ni vikundi hewa na ndiyo maana vingi vilishindwa,mfano Halmashauri hii ya Kishapu vikundi 31 vimeshindwa kurejesha Sh190 Milioni ambazo vilipatiwa vikundi hivyo”amesema Mkuu wa Mkoa

Ametumia fursa hiyo kuwataka vijana kuacha kutumia fedha za mikopo walizopewa na Halmashauri kwenda kucheza kamali,jambo ambalo wakibainika watachukuliwa hatua kali za kisheria ili kukomesha matumizi mabaya ya fedha ambazo zinatolewa na serikali.

Kwa upande wake Katibu wa kamati ya huduma za mikopo Wilaya ya Kishapu Joseph Swalala,amesema walipokea maombi 162 ya mikopo ambapo vikundi 102 vilikidhi vigezo ambapo kati ya hivyo vilivyopatiwa mkopo awamu ya kwanza ni vikundi 59.

Amesema vikundi 59 ambavyo vimepitishwa awamu ya kwanza 35 vya wanawake,22 vijana na viwili vya walemavu ambapo fedha zitakazotolewa ni Sh587.5 milioni lengo likiwa ni kuhakikisha mikopo hiyo inaleta tija kwa wananchi.

Baadhi ya wanufaika wa mikopo ya Halmashauri akiwemo Rehema John mkazi wa Kishapu,amesema mikopo waliyoipata watakwenda kuitumia vizuri kwa malengo yaliyokusudiwa ili kuwawezesha kurejesha fedha walizopewa kwa wakati.

Paul Juma mkazi wa Kata ya Mwamalasa amesema wanaishukuru serikali kwa kuwajali vijana ili wajikwamuwe kiuchumi kwa kufanya miradi ya kilimo na ufugaji,ambapo amesema serikali imesikia kilio chao kuwapatia mikopo ambayo italeta tija.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *