Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan amewataka Wanawake waliobahatika kupata fursa ya elimu na kuwa Viongozi kwenye maeneo mbalimbali, kuhakikisha wanafanya kazi kwa bidii, weledi na uadilifu, ili kuongeza imani kwa
jamii kuhusu umuhimu wa elimu kwa mtoto wa kike.
Rais Dkt. Samia ametoa wito huo hii leo Februari 21, 2025 kwenye maadhimisho ya miaka 10 tangu kuanza kwa Mafunzo
ya Uongozi kwa Wanawake Tanzania (Female Future Program), sambamba na Mahafali ya Wahitimu wa Awamu ya 10 ya Mafunzo hayo na Mkutano wa 7 wa Uongozi, yaliyofanyika jijini Dar es Salaam.

Amesema, wahitimu hao wanatakiwa kuwa chachu ya maendeleo katika jamii na kutumia elimu na stadi za uongozi walizopata kunufaisha jamii kwa ujumla.
Vilevile, Rais Dkt. Samia pia amewarai Wanawake kudhihirisha ushupavu wa uongozi kwenye Mashirika na Taasisi mbalimbali na kuwataka kuwa wabunifu kwenye kazi zao na kuwa waaminifu
katika kulipa kodi, ili kuwezesha utekelezaji wa miradi mbalimbali inayogusa maisha ya Mwananchi.

Katika kuhakikisha ustawi wa jamii, Rais Dkt. Samia amewahusia kuwa pamoja na elimu na nafasi za uongozi walizonazo, wasiache wajibu wao wa kijamii wa malezi na makuzi ya watoto ili kuwaepusha kujiingiza kwenye mienendo isiyofaa.
Kuhusu Uchaguzi Mkuu ujao, Rais Dkt. Samia amewahamasisha wanawake wenye sifa na uwezo kujiandikisha kupiga kura na kujitokeza kuwania nafasi mbalimbali.
