WANAWAKE CHANGAMKIENI FURSA KUJIIMARISHA KIUCHUMI -RC MACHA

Na Eunice Kanumba – Shinyanga.

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha amewasihi Wanawake na wasichana mkoani Shinyanga kujitokeza kwa wingi kushiriki katika fursa mbalimbali za kiuchumi na ujasiriamali zinazojitokeza, ili kujiimarisha kiuchumi.

Macha ameyasema hayo kwenye Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ambayo kimkoa yamefanyika Kata ya Bugarama, Halmashauri ya Msalala Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga, na kuhudhuriwa na Viongozi wa Taasisi za Serikali na Binafsi, Watumishi pamoja na Wanachi.

Amesema, “nichukue fursa hii kuwahimiza wanawake na wasichana wote kujitokeza kushiriki katika fursa mbalimbali za kiuchumi na ujasiriamali  zinazojitokeza ili kujiimarisha kiuchumi,.”

Aidha RC Macha ameongeza kwa kuwasihi wananawake kutumia nishati safi ya gesi na umeme ili kuunga mkono jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuifanya Tanzania iwe na matumizi ya nishati safi na utunzaji wa mazingira.

Akiwasilisha taarifa fupi ya shughuli zilizofanyika kwenye Maadhimisho ya Siku ya Wanawake kwa siku 3, Afisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Shinyanga, Rehema Edson amesema wameshirikiana na wajasiriamali 15, Taasisi takribani 9 zimeshiriki maonesho na kutoa huduma na kutekeleza  zoezi la ugawaji miti.

Miti hiyo itatumika kwa lengo la kutunza mazingira pamoja na kongamano kubwa la Wanawake takribani 466 walihudhuria na kupata elimu ya masuala mbalimbali ya kiuchumi na kijamii.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jukwaa la Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi mkoani Shinyanga, Dkt. Regina Malima ameshauri kuanzishwa kwa sera na mikakati ya kuwakwamua wanawake na wasichana kiuchumi sambamba na utoaji elimu endelevu ili wafahamu fursa zilizopo za kuwawezesha kiuchumi.

Maadhimisho ya Siku ya Wanawake mkoani Shinyanga, yaliambatana na shughuli mbalimbali ikiwemo maandamano, kutembelea mabanda ya maonesho pamoja na utoaji hundi za mikopo ya Serikali ya asilimia 10 kwa vikundi kwenye Halmashauri, yakiwa na kauli mbiu isemayo “Wanawake na Wasichana 2025: Tuimarishe Haki, Usawa na Uwezeshaji.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *