Wananchi wa Mkoa wa Mwanza wametakiwa kufuata sheria za zimamoto na uokoaji ili kuepuka matatizo yanayoweza kutokea kutokana na ukiukwaji wa sheria hizo.
Rai hiyo imetolewa na Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Mwanza, SSP. Elisa Mugisha wakati akizungumza na vyombo vya habari hii leo ambapo amesema mpaka sasa jeshi hilo limewashtaki jumla ya watu 47 kwa tuhuma mbalimbali zinazohusiana na kukiuka sheria hizo.
Mugisha amesema makosa yanayowakabili washitakiwa ni pamoja na kufanya biashara bila kuwa na cheti cha kuzuia majanga ya moto, kushindwa kutekeleza maagizo ya jeshi hilo na kujenga bila kupitisha ramani kwa idhini ya jeshi.

“Makosa yanayowapelekea kwenda mahakamani ningependa wananchi na umma wote wajue ni makosa ya kuvunja sheria za Zimamoto na Uokoaji kwahiyo mtu mmoja anaweza kuwa na tuhuma moja hadi tano na zilizonyingi ni kufanya biashara bila kuwa cheti cha majanga ya moto, pili kushindwa kutekeleza yale uliyoambiwa, lakini wengine ni wale ambao wanajenga bila kupitisha ramani au mali zao Jeshi la Zimamoto na Uokoaji,” amesema Mugisha
Mugisha amesema miongoni mwa walioshtakiwa ni kampuni ya Imalaseko Investment, ambayo inamiliki Nyumba ya mapumziko (Resort), Mohamed Kumalija mmiliki wa Kumalija Lodge, Hamis Sudi na Robert Mageyane wote kesi zipo mahakamani.
“Miongoni mwa waliokamatwa ni kampuni ya Imalaseko Investment, ambayo inamiliki sehemu ya mapumziko (resort) na imekuwa ikisumbua jeshi hilo kwa miaka miwili. Kampuni hiyo ilishawahi kufikishwa mahakamani na jana ilihukumiwa tena kwa kukiuka sheria za zimamoto. Aidha, Mohamed Kumalija, mmiliki wa Kumalija Lodge, amefikishwa mahakamani kwa mara ya pili kwa kosa la kutosifu.

Katika hatua nyingine, Mugisha pia amewataka wananchi wa mkoa huo kuhakikisha wanapeleka ramani za nyumba zao kwa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kabla ya kuanza ujenzi kwani hii inasaidia kuhakikisha majengo yanayojengwa yanakidhi viwango vya usalama na yanazingatia sheria za zimamoto.
Aidha pia amewaomba wananchi kuendelea kushirikiana na jeshi hilo ili kuhakikisha kila mmoja anakua salama yeye pamoja na mali zake.
“Tunawahimiza wote kushirikiana nasi kuhakikisha usalama wa maisha na mali zao,” amesema Mugisha.