Na Faustine Kasala – Kigoma.
Baadhi ya Viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo Chadema Mkoani Kigoma wametangaza kuachana na Chama hicho wakati wakitafakari jukwaa jipya la Kisiasa watakalo litumia kuendeleza harakati zao za kisiasa.
Wakizungumza na waandishi wa habari leo Mei 16, 2025 wakiongozwa na aliyekuwa Katibu wa CHADEMA Wilaya ya Kigoma Mjini, Deogratius Liyunga wamesema wameamua kuhama Chama hicho kutokana na mwenendo usioridhisha ndani ya Chama hasa kwa Viongozi waliojulikana ‘Timu Mwamba’ ambaye alikuwa mwenyekiti wa Chama hicho Taifa Freeman Mbowe.
Liyunga amesema anaondoka katika Chama alichokitumikia kwa zaidi ya miaka ishirini huku akilaumu Viongozi wa juu kukiua Chama.

“Baada ya Uchaguzi Mlimani City sisi Timu Mwamba tumekuwa tukiandamwa sana kila ukitoa maoni au ushauri hausikilizwi sasa imebaki tunapokea maelekezo kutoka juu hakuna haki katika Chama ambacho nimekitumikia kwa mda mrefu”alisema Liyunga.
Ameongeza kuwa Lisu baada ya kushinda uchaguzi alisema itakuja laki moja kila Jimbo na alituaminisha kuwa Chama kina fedha lakini tunashangaa akiwa Mbeya kwenye Mkutano tulipokea barua ya kuandaa Mkutano aliotakiwa kuja kabla ya kukamatwa na tukaambiwa tuchange kubeba gharama za Mkutano jambo ambalo amesema ni ubabaishaji wa mapema ndani ya chama.
Wengine waliotangaza kujiengua katika Chama hicho ni Mwenyekiti wa Baraza la wanawake Chadema (Bawacha) Mkoa wa Kigoma Hadija Ramadhan ambapo amelalamikia baadhi ya Viongozi wa Mkoa kumtuhumu kuwa yeye ni msaliti kwakuwa alikuwa upande wa Freeman Mbowe.

Aidha Hadija amesema kuwa kabla ya kujivua uanachama alishitushwa na taarfa ya mapema wiki hii kufukuzwa uongozi wa Bawacha na Makamu Mwenyekiti wa Chadema Mkoa kitu ambacho ni kinyume na katiba.
Ameongeza kuwa amekuwa akisimangwa kuwa amepokea fedha kwà ajili ya kugawa na kuwashawishi wanachama wa Jimbo la Kigoma Kusini ambako pia aliwahi kuongoza Bawacha katika wilaya ya Uvinza jambo ambalo amesema siyo sahihi.
Dismas Wiston aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Jimbo la Kigoma Kaskazini ametangaza pia kuachana na Chama hicho huku akieleza kusikitishwa kutuhumiwa na Katibu wa chama hicho mkoa kwa upotevu wa pikipiki ya Chama huku akidai kuwa amekuwa akitumia gharama zake binafsi kukijenga chama katika maeneo mbalimbali.

Katika Mkutano huo Viongozi wa Chama hicho waliotangaza kujivua uanachama wanatokea katika majimbo matatu ya uchaguzi Katika Jimbo la Kigoma Mjini, Kigoma Kaskazini na Kigoma Kusini.
Viongozi wengine waliotangaza kujiondoa ndani ya Chadema ni mhasibu wa Baraza la vijana Chadema (Bavicha) Jimbo la Kigoma Kusini ni Epifania Alex ambaye pia alikuwa mhasibu Bavicha kanda ya Magharibi,Iman Nassoro Mwenyekiti Bavicha Jimbo la Kigoma kusini, Faraji Tumain Mwenyekiti kata ya mwanga na mjumbe Halimashauri kuu Jimbo,Abdul Galula Katibu wa Bavicha Kigoma Mjini.
Aidha wengine waliotangaza kujivua uanachama ni Viongozi wa Kata zilizopo katika majimbo ya Kigoma Mjini,Kigoma Kaskazini na Kigoma Kusini ambapo wamesema kuwa wanapumuzika siasa huku wakitafakari jukwaa sahihi litakalowapa nafasi ya kufanya siasa safi na demokrasia tofauti na walipokuwa.


