‘WALIONG’OA VITI UWANJA WA MKAPA WAKAMATWE, POLISI WAPEWE USHIRIKIANO’ – WAZIRI KABUDI.


Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo imesema imesikitishwa na vitendo vya mashabiki kung’oa na kuharibu viti vya kukalia watazamaji katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam katika mchezo wa kugombea Kombe la Shirikisho Barani Afrika kati ya Simba Sport Club ya Tanzania na Club Sportif Sfaxien ya Tunisia mchezo uliochezwa jana tarehe 15 Desemba, 2024.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mheshimiwa Prof. Palamagamba Kabudi amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Gerson Msigwa kuchukua hatua mara moja kwa kuwaandikia timu ya Simba Sports Club na kuwanakili Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ili gharama za uharibifu uliosababishwa wakati mechi hiyo zilipwe.

Mheshimiwa Waziri Kabudi pia amewataka mashabiki wanaoingia katika Uwanja wa
Benjamin Mkapa kuacha vitendo vya uharibifu wa uwanja kwa kuwa wanasababisha hasara kwa Serikali na kuharibu ubora wa uwanja.

“Vitendo vilivyofanyika jana katika Uwanja wa Benjamin Mkapa havikubariki na sio vya kimichezo, nakuelekeza Katibu Mkuu kuchukua hatua mara moja. Pamoja na kuwaandikia Simba Sports Club na TFF, wapeni shirikiano Polisi ili watu wote waliokuwa wanang’oa viti na kuvitupa wakamatwe na wachukuliwe hatua za kisheria, lazima tabia hii ikomeshwe” amesema Prof. Kabudi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *