Utayari wa vyombo vya habari katika ushiriki wa kampeni mbalimbali za kitaifa ikiwemo uhamasishaji wa ushiriki wa jamii katika sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 umetajwa kuwa ni chachu ya kufikiwa kwa malengo ya kampeni mbalimbali za kitaifa.
Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Bi. Christina Mndeme amebainisha hayo Desemba 18,2023 katika ukumbi wa hoteli ya Karena Manispaa ya Shinyanga wakati akifungua semina ya mafunzo kwa waandishi wa habari inayohusiana na namna ya uwasilishaji,usambazaji na uhamashishaji wa matumizi ya matokeo ya sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 na kutoa pongezi kwa waandishi wote wa habari nchini.
Kwa Upande wake Kamishina wa Sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 Bi.Anne Makinda amesema kwamba ni matarajio yake kwamba mara baada ya mafunzo hayo ya siku mbili kukamilika,waandishi wa habari wataandika taarifa sahihi zinazohusu takwimu hatua iyakayowezesha wananchi wa kawaida kujua haki zao kwa mujibu wa Takwimu.
Akizungumza kwa niaba ya waandishi wa habari wanaoshiriki mafunzo hayo,Mwenyekiti wa klabu ya waandishi wa habari Mkoa wa Shinyanga Bw. Greyson Kakuru ameishukuru Ofisi ya Taifa ya Takwimu(NBS)kwa kuendesha mafunzo hayo na kueleza kwamba yatakuwa msaada mkubwa kwa waandishi wa habari katika utekelezaji wa majukumu yao. Mafunzo hayo yanaendeshwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu(NBS) yanafanyika kwa siku mbili yanatolewa kwa waandishi wa habari 120 ambao ni wanachama wa Klabu za waandishi wa habari kutoka mikoa ya Geita,Simiyu,Shinyanga na Tabora.